Machafuko yamtisha Nyagawa Comoro

Muktasari:

Kiungo huyo anaamini kuwa timu yake ina nafasi ya kupata mafanikio msimu huu wa ligi.

HOFU ya machafuko Comoro imeanza kumtisha Mtanzania, Boniface Nyagawa anayeichezea USZ Bonbon Ndjema kwa kusema pamoja na kuingia kwenye duru la pili la ligi, nafsi yake imepoteza amani.

Nyagawa alisema Comoros kuna vuguvugu la uwepo wa machafuko ya kisiasa kutokana na madai ya wanachi wengi kutovutiwa na uongozi wa Azali Assoumani.

“Umetoka kufanyika uchaguzi na inadaiwa rais wa sasa anataka kuendelea kuwapo kwenye nafasi hiyo, naogopa sana vurugu huku ni ugenini na wanaweza kutuweka pabaya wageni kwa kudhani sisi ndiyo wachochezi.

“Naomba Mungu hili lipite ili maisha mengine yaendelee kwa amani.

“Tulicheza mchezo wetu wa ligi juzi (Jumamosi) dhidi ya Walla FC na nashukuru Mungu tulishinda kwa mabao 3-1,” alisema kiungo huyo mkabaji.

Nyagawa aliongeza: “Ushindi huo tulioanza nao duru la pili naamini ni mwanzo mzuri kwetu kwenye mchakato wa kutaka tumalize vizuri msimu kwa kutwaa ubingwa.”

Kiungo huyo anaamini kuwa timu yake ina nafasi ya kupata mafanikio msimu huu wa ligi.