Mabeki, washambuliaji watia hofu kocha Singida Utd

Thursday August 9 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Benchi la Ufundi la Singida United limesema bado wanakazi kubwa ya kufanya katika safu ya beki na ushambuliaji kabla ya kuanza Ligi Kuu msimu huu.

Akizungumza baada ya kushuhudia timu yake ya Singida United ikilazimishwa sare 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Nyamagana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jumanne Challe alisema bado hajakubali kiwango cha vijana wake.

Alisema kuwa licha ya kwamba wanaweza kufanya kitu hapo baadaye, lakini kwa sasa anapaswa kufanyia kazi safu yake ya ushambuliaji na beki kabla ya kuanza Ligi Kuu Agosti 22.

“Bado safu yangu ya ulinzi haijawa fiti pamoja na ushambuliaji, lakini kupitia mashindano haya naamini kikosi change kitafanya vizuri na kuweza kutwaa Ubingwa”alisema Challe.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema kuwa licha ya mapungufu yaliyopo kikosini kwake anaamini kabla ya Ligi kuanza vijana wake watakuwa tayari kuhimiri mikiki mikiki.

“Vijana wanabadirika japo bado mapungufu yapo ndio maana nawapima mmoja mmoja hapa ili kuhakikisha Ligi itakapoanza wawe tayari kiushindani”alisema Mexime.

Katika mtanange huo, Singida ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 60 kupitia kwa Eliuta Mpepo kwa penalti, kabla ya Kagera kusawazisha kupitia kwa David Luhende kwa penalti dakika ya 79.

Advertisement