Mabao ya Dube, yamshtua Kagere

PRINCE Dube juzi usiku alifunga bao lake la sita msimu huu katika Ligi Kuu Bara, akiwa na wastani wa bao moja kila mechi, jambo ambalo limemfanya Mfungaji Bora kwa misimu miwili iliyopita, Meddie Kagere kushindwa kujizuia na kumzungumzia straika huyo wa Azam FC.

Dube alifunga bao hilo wakati Azam ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Azam Complex na kumfanya aendelee kubaki kileleni akiwa na mabao sita akimzidi hata Kagere mwenye mabao manne na straika huyo kutoka Rwanda alifunguka juu ya kasi ya Dube.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Kagere amesema kiwango kinachoonyeshwa na Dube katika ufungaji kinasaidia kuongeza ushindani kwa mastraika wote waliopo katika timu 18 za ligi hiyo na kudai kwake imekuwa changamoto inayomfanya azidi kujipanga zaidi msimu huu.

Kagere alisema Dube amemkumbusha kuwa hapaswi kubweteka baada ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo akiweka rekodi na kudai hata alipotua nchini kwa mara ya kwanza kutoka Kenya alikumbana na changamoto kama hiyo kutoka kwa Heritier Makambo aliyekuwa Yanga.

“Nimeanza msimu kwa kuweka malengo, kwanza kutoa mcha-ngo na kuisadia timu ili kuchukua mataji mbalimbali lakini pia nikitamani kutwaa tena tuzo kwa msimu wa tatu mfululizo, naamini Dube ameongeza kitu kwenye malengo yangu kuwa, sitakiwi kubweteka,” alisema Kagere na kuongeza;

“Dube na Obrey Chirwa (aliyefikisha idadi ya mabao manne kama ya Kagere) wananifanya nijipange kwani vita ya ufungaji msimu huu inaweza kuwa kubwa kuliko misimu miwili iliyopita, hii ni dalili nzuri imeanza kuonekana mapema kutokana na ubora wao.

“Nakumbuka nilipoanza kucheza ligi hapa nchini nilikutana na ushindani kama huo kutoka kwa Heritier Makambo na Eliud Ambokile aliyekuwa Mbeya City, ila nikatimiza majukumu yangu ya kufunga zaidi na kutwaa kiatu kwa mabao 23 na kuipa pia timu yangu ubingwa wa Ligi Kuu,” alisema.

MHILU, ABRAHAM MOTO

Licha ya orodha ya wafungaji kwa sasa kuongozwa na wageni watupu, lakini kuna wazawa wawili wanaowatoa jasho wageni hao akiwamo Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar na Meshack Abraham wa Gwambina FC wenye mabao matatu kila mmoja sawa na Chris Mugalu wa Simba na Blaise Bigirimana wa Namungo.

Mhilu anaonekana ndiye kiboko yao kwani licha ya kukosa mechi tatu za awali za timu yake, kwenye mechi nyingine tatu zilizofuata amefunga mfululizo na kufikisha mabao hayo, huku akiwa pia ndiye kinara wa msimu uliopita kwa wazawa kwa kufunga mabao 13.

Akizungumzia kasi yake Mhilu aliyewahi kukipiga Yanga na Ndanda, alisema; “Unajua kufunga ni uwezo wa kutumia nafasi ambazo zinapatikana uwanjani kwa maana hiyo huwa nakuwa mtulivu kila ambapo napata nafasi hiyo ili kuitumia vyema kufunga bao ndio maana mpaka sasa nimefanikiwa kufunga matatu ingawa nilikuwa na uwezo wa kufanya hivyo kwani nilipoteza nafasi nyingine.

“Siwezi kueleza naweza kuwa mfungaji bora wa ligi kwani ndio kwanza inaanza na katika soka lolote linaweza kutokea kwa maana hiyo nitakuwa natimiza majukumu yangu ili kuisaidia timu nami niendelee kukomaa na wageni ambao wametwaa tuzo ya ufungaji misimu mitatu mfululizo sasa.”