Mabao 10 matamu Ligi Kuu

Muktasari:

Singida United Hii ndiyo timu ya kwanza kushuka daraja msimu  huu, ilifungwa  mabao 73 na ikafunga 23.

MABAO ni kitu cha muhimu ambacho huamua matokeo ya mchezo wa soka uwanjani.

Mara nyingi mabao hufungwa na wachezaji wanaocheza katika safu ya ushambuliaji, lakini hata wachezaji wa nafasi nyingine wamekuwa wakizifumania nyavu pale wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.

Hata hivyo ni jambo la kuvutia pale mchezaji anapofunga goli kwa namna ya kipekee na ya kusisimua jambo ambalo huongeza ladha kwa watazamaji wa mchezo wa soka.

Katika Ligi Kuu msimu huu, wapo wachezaji ambao wamefunga mabao matamu ambayo yamekuwa gumzo kwa mashabiki na wapenzi wa soka ambao wamekuwa wakifuatilia ligi hiyo.

Ifuatayo ni orodha ya mabao 10 yaliyofungwa katika Ligi Kuu msimu huu ambayo staili ya ufungwaji wake nimeona ilikuwa ya kipekee na hapana shaka yanakuwa bora.

Hata hivyo orodha hiyo haijapangwa kwa mtiririko wa kumaanisha ya mwanzoni kutajwa ndio bora zaidi kulinganisha na yale ya mwishoni.

Lucas Kikoti - (Simba vs Namungo)

Shomary Kapombe aliokoa mpira wa kichwa ambao ulinaswa na mshambuliaji wa Namungo Reliants Lusajo ambaye alifanya uamuzi wa haraka wa kumpasia kiungo Lucas Kikoti aliyekuwa mbele ya wachezaji wawili wa Simba.

Mara baada ya kupokea mpira huo, Kikoti alichokifanya ni kujitengea na kupiga shuti kali la mguu wa kulia ambalo lilikwenda moja kwa moja wavuni na kuipatia Namungo bao la pili la kusawazisha ingawa walipoteza mechi hiyo kwa mabao 3-2.

David Molinga -(Yanga vs Polisi)

Yanga ilikuwa nyuma kwa mabao 3-2 dhidi ya Polisi Tanzania lakini iliokolewa na mkwaju wa faulo wa mshambuliaji aliyeingia kutokea benchi, David Molinga.

Mshambuliaji huyo alipiga faulo maridadi ya mguu wa kulia akiupeleka mpira pembeni ya wachezaji wa Polisi Tanzania waliokuwa wamepanga ukuta na kuujaza wavuni.

George Makang’a - (Lipuli vs Namungo)

Winga George Makang’a alipokea pasi fupi upande wa kushoto kutoka kwa Edward Manyama na pasipo kuchelewa alipiga mpira kwa staili ya kuuzungusha kwenda katika kona ya kushoto ya lango la Lipuli na kuipatia Namungo FC bao la pili.

Hassan Dilunga - (Simba vs Namungo)

Akiwa upande wa kulia, Hassan Dilunga alipokea pasi kutoka kwa Meddie Kagere na kisha kuwahadaa walinzi wawili wa Namungo FC kisha akakata kuelekea upande wa kulia wa lango la wapinzani wao.

Ghafla Dilunga alichukua uamuzi wa haraka wa kupiga shuti kali la mguu wa kushoto ambalo lilimshinda kipa Nurdin Balora na kujaa nyavuni akiiandikia Simba, bao la pili.

Bernard Morrison - (Yanga vs Simba)

Jonas Mkude alifanya kosa la kumfanyia madhambi, winga Bernard Morrison wa Yanga ambaye alikuwa anakatiza na mpira kutoka winga ya kulia kueleka kushoto jambo lililomfanya mwamuzi Martin Saanya kupiga filimbi ya kuashiria pigo la faulo.

Morrison aliitazama vyema ukuta uliopangwa na wachezaji wa Simba na kupiga faulo hiyo iliyopita juu yao na kuzama kwenye kona ya lango la wapinzani wao na kuiandikia Yanga, bao pekee la ushindi katika mchezo huo.

Yakubu Mohamed - (Mbao vs Azam)

Akiwa nje ya eneo la hatari la Mbao FC, beki Yakubu Mohamed aliupokea vyema kwa kifua mpira uliookolewa kwa kichwa na beki wa wapinzani wao na kuwahadaa wachezaji wawili wa Mbao FC.

Nyota huyo wa Ghana anayecheza nafasi ya beki wa kati, alichokifanya ni kupiga shuti la wastani ambalo lilikwenda moja kwa moja langoni mwa Mbao na kuipa Azam FC bao pekee la ushindi katikamchezo huo.

Mapinduzi Balama - (Simba vs Yanga)

Wakati Simba ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0, kiungo Mapinduzi Balama alifanikiwa kuupora mpira kwa Mzamiru Yassin wa Simba na kusogea nao kidogo kisha kupiga shuti kali la mguu wa kulia lililomshinda kipa Aishi Manula na kujaa wavuni.

Bao hil lilionekana kuirudisha Yanga mchezoni kwani baadaye ilisawazisha na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare ya mabao 2-2.

Luis Miquissone - (Simba vs Alliance)

Clatous Chama alimpigia pasi maridadi, Luis Miquissone aliyekuwa upande wa kushoto wa lango la Alliance.

Nyota huyo kutoka Msumbiji aliutuliza vyema mpira huo na kuwatoka walinzi wawili wa timu pinzani huku akikatiza kuelekea kulia kwa lango na kupiga mpira kwa staili ya kuzungusha akitumia mguu wake wa kushoto ambao ulikwenda moja kwa moja nyavuni na kuiandikia timu yake bao la tatu katika mchezo huo ambao waliibuka n ushindi wa mabao 5-1.

Israel Patrick - (Alliance vs Ndanda)

Mlinzi mmoja wa Ndanda FC alinawa mpira nje kidogo ya lango lake na kupelekea mwamuzi kuamuru pigo la faulo ambalo lilitumiwa vyema na nahodha wa Alliance, Israel Patrick kuiandikia timu yake bao la pili. Beki huyo wa kulia wa Alliance aliwazuga wachezaji wa Ndanda waliokuwa wamepanga ukuta kwa kufanya kama anataka kuuinua mpira kuelekea upande wao wa kulia na kuupenyeza upande wao wa kushoto ambao ulikuwa wazi na akaujaza wavuni.

Michael Aidan - (JKT Tanzania vs Yanga)

Beki wa kulia wa JKT Tanzania, Michael Aidan alipokea mpira akiwa mbele kidogo ya mstari wa kati wa Uwanja wa Jamhuri na kufunga goli ambalo limekuwa gumzo katika Ligi Kuu msimu huu.

Aidan alipiga mpira mrefu wa juu ambao ulimshinda kipa Metacha Mnata wa Yanga na kwenda kutinga wavuni akiipatia timu yake bao la kuongoza katika mchezo huo ambao hata hivyo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.