MTU WA PWANI : Musonye anahitaji darasa la hesabu na soka

Saturday July 27 2019

 

By Charles Abel

KUNA haja kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye kurudi upya darasani na kusoma somo la hisabati.

Na baada ya hapo atafute mwalimu mzuri ambaye atamfundisha na kumpa darasa la mchezo wa mpira wa miguu tofauti na alivyo kwa sasa. Mweupe kabisa.

Kauli za kashfa na kejeli ambazo anaendelea kuzitoa kwa klabu za Simba na Yanga mara baada ya timu hizo kuamua kutoshiriki maahindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kidogo zinanipa shaka naye.

Ni kama zinatolewa na mtu ambaye ameshindwa kuwa na uwezo wa kupiga hesabu rahisi au asiyefahamu chochote kuhusu mchezo wa soka.

Kama angekuwa anafahamu vizuri hesabu, Musonye angefahamu kwamba Yanga na Simba zilikuwa na mantiki kwa kutoshiriki mashindano ya Kagame ambayo yamemalizika huko Rwanda wiki iliyopita.

Bingwa wa mashindano ya Kagame mwaka huu, timu ya KCCA kutoka Uganda, imepata zawadi ya kombe na kitita cha Dola 30,000 (zaidi ya Sh 69 milioni) baada ya kucheza mechi sita za mashindano hayo.

Advertisement

Lakini, wakati huohuo timu ambayo inafanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga na Simba zitashiriki msimu ujao, inakuwa imejihakikishia kitita Cha Dola 550,000 (zaidi ya Sh 1.2 bilioni) hata kama itashika mkia kwenye kundi lake.

Ili ufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utalazimika kucheza mechi nne tu ambazo kama ukipata matokeo mazuri unakuwa umefuzu na kuzoa kitita hicho cha zaidi ya Sh 1.2 bilioni.

Nahisi Musonye hakupiga hesabu hizi. Inashangaza kidogo kuona anazikejeli timu ambazo zimeamua kuingia msituni kuhakikisha zinapata ushindi kwenye mechi nne ili zivune Sh 1.2 bilioni na badala yake anataka zikashiriki mashindano ambayo zitalazimika kucheza mechi sita (6) kwa ajili ya kupata Sh 69 milioni.

Kiufupi fedha ambazo Simba na Yanga kila moja itaingiza kwa kutinga hatua ya makundi baada ya kucheza mechi nne, ni zaidi ya mara 18 ya fedha ambazo bingwa wa Kagame anapata baada ya kucheza mechi sita.

Tathmini ya harakaharaka inaonyesha kuwa fedha ambayo timu inayoshika nafasi ya mwisho kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inatosha kuandaa na kugharamia mashindano ya Kagame kwa miaka mitano mfululizo.

Hapa Musonye anakosa hoja ya msingi ya kuzilaumu na kuzikejeli Yanga na Simba. Hatua ya makundi ambayo Simba na Yanga wanaifikiria zaidi, sio tu ni ya juu na yenye heshima kubwa zaidi bali pia inaziingizia klabu fungu kubwa la fedha ambalo linasahaulisha kabisa hadithi ya mashindano ya Kagame.

Lakini, pia inawezekana darasa la soka limepita kushoto kwa Musonye au anafanya kusudi kuziponda Yanga na Simba ama ameamua tu kuzishambulia kwa utashi wake kumaliza hasira alizonazo kwa kukosa viingilio vya mashabiki kutokana na timu hizo kutoshiriki kwenye mashindano yake. Kama kiongozi unapaswa kupima kila kitu kabla ya kuzungumza kwenye hadhara. Hili nalo linahitaji darasa kwa Musonye?

Mashindano ya Kagame mwaka huu yamekuja katika kipindi ambacho timu zimekuwa zikifanya usajili kwa kuingiza nyota wapya kikosini na kuondoa baadhi ambao, wameshindwa kuonyesha kiwango bora msimu uliopita.

Kwa maana hiyo klabu zilihitaji muda wa kufanya maandalizi na kutengeneza muunganiko wa kitimu kisha ndipo zianze kucheza mechi za kimashindano badala ya kutumia mashindano kujenga kikosi.

KCCA ambayo imetwaa ubingwa, kwa kiasi kikubwa imenufaika na kuwa na kikosi kilichokaa pamoja muda mrefu tofauti na timu nyingine zilizoshiriki mashindano hayo ambazo ndio zimetoka kufanya na zinaendelea na usajili.

Hapa kuna mawili. Kwanza timu zinaweza kutoleta ushindani wa kutosha kwenye mashindano kwani, zitaingia na vikosi ambavyo havina muunganiko mzuri lakini pia inaweza kuziumiza timu kwenye mashindano ya kimataifa kwa wachezaji kutopata muda wa kutosha kujiandaa na kupumzika kuelekea mashindano hayo.

Musonye kama Mtendaji Mkuu wa CECAFA ambao ni chombo kinachosimamia mpira wa miguu ukanda wa Afrika Mashariki na Kati anapaswa kujivunia kwa mafanikio ya timu na klabu za ukanda huu kwenye mashindano ya Afrika badala ya kutazama maslahi yake mwenyewe.

Haipendezi kuona kila mwaka timu za ukanda wa Afrika Mashariki zikiwa zinasindikiza mashindano ya kimataifa huku zikiacha zile za kanda zingine zikitamba.

Yeye kama mtendaji anatakiwa kuwa dira ya mafanikio ya timu za ukanda huu badala ya kugeuka adui.

Kitendo cha kila wakati Musonye kusimama na kuzungumza maneno yale yale ya kejeli kwa Simba na Yanga, kinaleta ukakasi miongoni mwa wadau wa soka na kuhisi kama anaendesha mambo kwa ajenda zake binafsi na si maneno ya kiongozi wa soka.

Advertisement