MSHTUKO!Mo Dewji atekwa kimafia Dar

Muktasari:

  • Mo alitekwa jana asubuhi akiwa anaelekea kwenye mazoezi katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

MSHTUKO mkubwa umeipata Tanzania, hususani mashabiki wa soka. Hii ni baada ya Bilionea wa klabu ya Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji kutekwa kininja na watu wasiojulikana wakati akiwa hotelini anakoenda kufanyia maozezi ya viungo kila siku.

Taarifa hizo zilienea mapema asubuhi na baadaye ilifahamika kwamba bilionea huyo ambaye bado haijulikani alipo alitekwa na Wazungu ambao walihusika katika ramani nzima.

Tukio hilo limeleta taharuki kubwa sio kwa mashabiki wa Simba, bali wanamichezo kwa ujumla, viongozi wa serikali na wanasiasa, ikiwa ni tukio la kwanza la kutekwa kwa mwanamichezo, mfanyabiashara na bilionea kama MO Dewji nchini Tanzania, japo vitendo vya utekaji vimekuwa vikijitokeza kwa siku za karibuni nchini ikiwamo la watoto wadogo.

 

TUKIO LILIVYOKUWA

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa MO waliliambia Mwanaspoti, mara baada ya Bilionea huyo kumaliza kuswali alfajiri jana alianza ratiba yake ikiwa ni kwenda hoteli ya Colloseum, iliyopo Oysterbay anakofanyia mazoezi kila siku.

Inaelezwa MO alifika hotelini hapo akiwa katika gari yake maalum nyeusi aina ya Range Rover yenye namba za usajili MO 1, kisha kushuka na kutaka kuingia ndani ya jengo la mazoezi (gym) kabla ya hekaheka hiyo kumkuta.

 

Polisi waeleza

ilivyokuwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alitoa taarifa baadaye kwa kusema kuwa, katika uchunguzi wao wa  awali kupitia kamera za ulinzi (CCTV) zimeonyesha magari mawili yalihusika. Mambosasa alilielezea tukio akisema  katika tukio hilo magari hayo mawili yalifika hotelini hapo kabla MO hajafika. Alisema gari ya kwanza aina ya Toyota Surf ilikuwa imeegeshwa nje ya geti la kuingilia hotelini likiangalia usawa wa ndani ya hoteli, huku la pili aina ya Toyota Noah likiegeshwa pembeni kidogo ya eneo ambalo MO hupaki gari lake kila afikapo hotelini na kushuka. Wakati Mo akifika hapo kamera zilionyesha gari ya ndani aina ya Noah ikiiwashia taa gari ya nje kuashiria kwamba MO amefika. Mara baada ya kuwasha taa hizo wakati Mo anashuka watu wawili raia wa kigeni (wazungu’) waliteremka na kuingia ndani ya geti la kuingilia kisha kukutana na MO akiwa anafunga gari yake na kuanza kuingia ndani ya jengo. Watu hao wawili walifika kwa Mo na kufanikiwa kumbana vizuri ambapo wakati wakiendelea na kazi hiyo gari iliyopaki nje ilikuwa imeshafanikiwa kuingia ndani ya geti na watekaji kufanikiwa kumuingiza katika gari iliyotoka nje aina ya Surf. Mara baada ya watekaji kufanikiwa walimpokonya funguo ya gari na simu yake kisha kuzitupa chini na kuanza safari ya kuondoka eneo hilo.

Kamera zilionyesha tukio hilo lilikamilika majira ya saa 11:35 alfajiri ambapo   wakati wanatoka Surf ambayo ilimbeba Mo ilitangulia mbele huku Noah ikifuata nyuma mpaka kwenye geti la kutokea. Walipofika hapo Wazungu hao alishuka mmoja na kufyatua risasi mbili juu kuamrisha mlinzi afungue geti ambapo wakati walinzi wakijisalimisha Mzungu aliyeshuka akakimbia getini na kufungua geti mwenyewe na gari zote kufanikiwa kukimbia.

MSAKO MKALI

Kamanda Mambosasa alisema kufuatia tukio hilo jeshi la polisi linaendesha msako mkubwa wakilenga kuwanasa wahusika, anafuatilia raia wa kigeni waliopo nchini na hata wengine katika kuhakikisha Mo anapatikana.

“Uchunguzi mkubwa unaonyesha tukio hili limewahusisha raia wa kigeni wawili ambao ni Wazungu na msako wetu huu tutaufanya kwa raia wa kigeni na wengine mpaka tuwapate wahusika,” alisema Mambosasa. “Tutapita kokote tutaingia kokote kuhakikisha tunampata Mo na wahusika tunawanasa na kuwashughulikia, niwaombe watu wote  wenye taarifa za kutusaidia jeshi la polisi wasaidie pia.”

IMEANDIKWA NA KHATIMU NAHEKA, EDO KUMWEMBE, MWANAHIBA RICHARD, OLIPA ASSA NA CHARITY JAMES.