MSHTUKO MKUBWA!

Friday October 12 2018

 

MSHTUKO mkubwa umeipata Tanzania, hususani mashabiki wa soka. Hii ni baada ya Bilionea wa klabu ya Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji kutekwa kininja na watu wasiojulikana wakati akiwa hotelini anakoenda kufanyia maozezi ya viungo kila siku.

MASWALI MAGUMU

Aidha Kamanda Mambosasa alisema kupitia tukio hilo watu watatu ambao ni wahusika katika hoteli hiyo wako katika uchunguzi kulisaidia jeshi la polisi.
Mambosasa alisema kufuatia tukio hilo kuna maswali yamekuwa yakiwasumbua, ambayo wanatafuta majibu yake na kuyakosa.
“Hebu tujiulize kamera nayo imeshindwa kutupatia kila kitu kuna upande tumeshindwa kuupata vizuri tunajiuliza ilikwepeshwa makusudi? 
Swali la pili hawa jamaa walifika mapema kabla ya MO lakini walikuwa hapahapa hotelini hawa walinzi wa hapa kwanini hawakuchukua hatua kuwauliza mbona ndugu zetu hamshuki kwenye gari?

Tatu tunaambiwa wakati zoezi linafanyika hakukupigwa yowe wala majibizano ya risasi ina maana hawa waliokuwa hapa walilichukuliaje tukio hili?

Swali lingine la mwisho hakuna aliyeandika gari zinazoingia kwahiyo hebu tufanye uchunguzi,” alisema Mambosasa.

 

KAULI YA MAKONDA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ambaye naye alifika katika eneo la tukio alisema tukio hilo limewashtua na kwamba MO ni raia mwema anayeishi ndani ya mkoa wake na watafanya uchunguzi wa kina.
Makonda alisema msako  utakaofanyika utawagusa watu wengi na nyumba nyingi mpaka kuhakikisha wanafanikiwa kujua ukweli.
“Hili ni tukio baya ambalo serikali haitalifanyia mzaha tutapita nyumba kwa nyumba lakini pia kila eneo ambalo litakuwa sehemu ya kutokea tutaweka ulinzi mkali hakuna atakayetoka bila kujiridhisha,” alisema Makonda.


MANARA AFICHUA

Afisa Habari wa Simba Haji Manara, aliyefika eneo hilo alisema Simba imeshtushwa na taarifa hiyo na kwamba wanaziachia mamlaka kutafuta alipo MO.

Manara alisema tukio hilo limetokea siku moja baada ya MO kusimamia kikao cha Bodi ya Simba kilichofanyika juzi.
Alisema MO wakati wote wa kikao hicho alionekama mchangamfu na mwenye furaha. Jambo hilo limewashtua wajumbe wenzake.
“Simba tumeshtushwa sana na tukio hili limetupa kiza kizito tusijue kipi kimemkumba mwenzetu,” alisema Mmanara akiwa katika uso wa huzuni.

“Mo tulikuwa naye jana (juzi) katika kikao cha bodi aliendesha kikao vizuri alikuwa mwenye furaha kama siku zote na kikao kilimalizika salama.“

Zinapokuja taarifa kama hizi zinasumbua lakini wanasimba wenzangu tuwe watulivu tumuombee mwenzetu huko aliko asipatwe na baya lolote, lakini pia tuwaachie jeshi la polisi na serikali kwa ujumla wenye mamlaka ya kulipatia ufumbuzi suala hili,” alisema.

TAARIFA ZACHANGANYA

Wakati polisi wakitawanyika katika eneo hilo dakika chache baadaye hali ilibadilika baada ya uvumi kuenea kwamba MO amepatikana na watekaji wamenaswa. 
Kusambaa wa taarifa hiyo kulionyesha kuwasumbua wengi huku watu wakifurika hotelini hapo kupata uhakika zaidi.
Baada ya taarifa hiyo ambayo haikuwa na ukweli ilimlazimu Makonda kurudi hotelini hapo na kukanusha taarifa hiyo.
“Ndugu zangu hizo taarifa kwamba MO amepatikana hazina ukweli ni watu wameamua kupotosha kwa madhumuni yao, kipindi hiki sio vizuri kila mmoja anaonekana kutoa taarifa na kusambaza,” alisema Makonda.

VIGOGO SIMBA WATUA

Baada ya saa moja vigogo  wazito wa Simba walifika hotelini hapo na kutaka kujua kilichoendelea. 
Baadhi ya waliofika hotelini hapo ni Crestecius Magori, Mulamu Nghambi na Mohamed Nassoro ambao hufanya kazi kwa karibu na MO.

 

NYUMBANI HUZUNI TUPU

Siku hiyo ya jana hali haikuwa nzuri kwa ndugu jamaa na marafiki wa MO ambao walionekana kutoka na kuingia nyumbani kwa MO. 
Katika mtaa wa Laibon nyumba na. 20 Oysterbay ambako ndiko Mo anaishi ulinzi ulikuwa mkubwa huku ndugu na jamaa wakionekana na hali ya simanzi.

Hakuna aliyekubali kuongea na Mwanaspoti lakini kila mmoja alionekana katika taharuki kubwa huku wakibadilishana mawazo.

IMEANDIKWA NA 
KHATIMU NAHEKA, EDO KUMWEMBE, MWANAHIBA RICHARD, OLIPA ASSA NA CHARITY JAMES.

Advertisement