MO Simba Awards zimeiva, tuzo 12 kutolewa

Thursday May 16 2019

 

By Thobias Sebastian

SIKU mbili mara baada ya Ligi Kuu Bara kumalizika Mei 30, katika Hoteli ya Hyatt Regency mabosi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' watatoa tuzo kwa wachezaji wao na vipengele vingine mbalimbali.

Akizungumzia hilo Msemaji wa tuzo hizo za 'MO Awards 2019'  Rabi Hume alisema sherehe itafanyika siku ya Mei 30, mara baada ya kumaliza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar ambao uatachezwa Uwanja wa Manungu Morogoro.

Hume alisema tukio hilo litafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency na kutakuwa na vipengele 12, katika sehemu mbalimbali ambazo zitawania na kila mshindi atapatikana siku hiyo baada ya kupigiwa kuru na wapenzi na wanachama kupitia mitandao yetu ya kijamii.

"Kutakuwa na vipengele 12, ambavyo ni kipa bora, beki bora, kiungo bora, mshambuliaji bora, goli bora la mwaka, mfungaji bora, tuzo ya wachezaji, mchezaji bora, tuzo ya heshima, shabiki bora, mchezaji bora mdogo na mchezaji bora wa kike," alisema.

"Mchezaji bora wa kike atapatikana katika timu yetu ya Simba Queens na ukiondoa mfungaji bora katika kila kipengele cha tuzo kutakuwa na wanaowania watatu na mmoja atapatikana kuwa ni mshindi," alisema Hume na kueleza shughuli hiyo itafanyika kuanzia saa 12:00 jioni.

Advertisement