MANYIKA JR: Ile dabi ya 2014 siyo mchezo

Tuesday May 12 2020

 

By YOHANA CHALLE

ULE usemi usemao “binadamu hukutana, ila milima haikutani” ulikuwa na maana kubwa katika maisha ya binadamu.

Ndivyo inavyokuwa kwa nyota wa Polisi Tanzania, Manyika Peter JR ambaye alitamba na kikosi cha Simba miaka ya nyuma kisha akatimkia Singida United na baadaye KCB ya Kenya.

Manyika Jr kwa sasa anapambana vilivyo katika kikosi hicho cha maafande akiwania namba mbele ya Mohamed Ali pamoja na Kurwa Manzi.

Mwanaspoti limepiga na stori na Manyika Jr aliyeanzia soka katika Klabu ya Zaragoza ya Magomeni, Dar es Salaam chini ya kocha anayemkumbuka kwa jina moja la Pereirra.

Baada ya hapo akajiunga na kituo cha kukuza vipaji cha Twalipo Youth Soccer Foundation na baadaye kujiunga na timu ya vijana ya JKT Ruvu U-20.

Hakuishia hapo kwani akatimkia Mgambo JKT, kisha kurudi kucheza Ligi Daraja la Pili (SDL) akiwa na Red Coast ya Mburahati na baadaye akajiunga na Boom FC ya Ilala safari iliyoendelea hadi Simba.

Advertisement

MAISHA NDANI YA SIMBA

“Maisha ndani ya Simba yalikuwa ambayo yamenifunza mengi na kunikomaza kikazi na kimaisha. Nimejifunza mambo mengi ya maisha ya ndani na nje ya mpira, Simba imenifanya kila ninalolifanya nijiamini,” anasema mchezaji huyo ambaye baba yake ni kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika.

Anasema changamoto kubwa aliyokumbana nayo Msimbazi ilikuwa ni kupata nafasi ya kucheza kutokana na walinda mlango aliowakuta akiwemo mkongwe, Ivo Mapunda.

“Ivo Mapunda kwangu alikuwa msaada mkubwa sana, maana alikuwa ananipa matumaini ya kufanya vizuri na kunijenga katika upande wa golini,” anasema.

“Kila ninapokosea uwanjani kaka Ivo alikuwa mbele kuniambia nini nilitakiwa kufanya ili niwe bora zaidi, alikuwa na mchango mkubwa sana na hata hapa nilipo siwezi kumsahau kutokana na mchango wake.”

Anaongeza kuwa aliondoka Simba kwa nia njema kwa sababu aliongea na viongozi kabla hajatoka na kuwaambia dhamira yake siku za usoni ilikuwa nini.

“Wakaniruhusu niende kutafuta changamoto nyingine ambayo kwa kiasi kikubwa niliipata na kurudi katika ubora nikiwa na Timu ya Singida United,” aliongeza huku akisema kilichompeleka na kumtoa Kenya.

KILICHOMKIMBIZA KENYA

“Ligi ya Kenya haionekani kokote na hamna koneksheni kubwa kama kipindi cha huko nyuma ilivyozoweleka palipokuwa na Supersport (kituo cha runinga).”

Hata hivyo, anasema dhamira yake ya kucheza soka la nje bado ipo: “Nafanya kazi kokote, kama mfanyakazi sitakuwa na pingamizi endapo watakubaliana na uongozi wa mahali nilipo (Polisi Tanzania) au nitakapokuwa chini ya meneja wangu.

“Baba yangu ndiye meneja wangu kwa kuwa yeye ndiye aliyenionyesha njia ya mpira na kuwa nami tangu naanza mpira wa ushindani na pia ameshaucheza mpira kwa kiwango kikubwa, hivyo naamini kile anachoniambia,” anasema.

SIMBA FRESHI

“Kama nilivyokuambia nafanya kazi sehemu yoyote kama uongozi wangu watakubaliana, kwangu sina tatizo kwani soka ndio kazi yangu.”

Kuhusu ushindani wa namba kwenye kikosi cha Sven Ludwig Vandenbroeck anasema: “Ushindani wa namba ni mzuri na naupenda sababu inakupa muda wa kujiweka sawa kila dakika na kila saa bila kujali unacheza au huchezi kwani hujui lini utaopata nafasi ya kusaidia timu.”

“Hata nilipokuwa Singida United niliondoka baada ya kupata ofa wakaniacha kwa makubaliano yangu na uongozi wa timu na kila kitu kikaenda sawa, ndio maisha ya soka yalivyo.”

AIKUMBUKA DABI

Oktoba 18, 2014 wakati Simba ikitoa suluhu Uwanja wa Taifa wengi walikuwa hawaamini kwa yale yaliyofanywa na Manyika JR akiwa na umri chini ya miaka 20.

Walinda mlango wa Simba; Ivo na Hussein Sharrif ‘Casillas’ wote walikuwa majeruhi ndipo dogo akaonyesha ubabe wake langoni ingawa kabla ya kuanza kwa mechi hiyo mashabiki wa Simba walionyesha hofu dhidi yake, lakini aliwatoa kimasomaso dhidi ya Yanga iliyokuwa imeshiba.

“Kabla ya dakika 90 hali kwangu ilikuwa sio hali kwasababu ni mechi kubwa ya watani na sikuwahi kucheza, ila baada ya kuingia uwanjani wakati wa kupasha misuli niliona hali ya kawaida na nikajipa moyo kuwa mechi itaisha tu na jua litachomoza kesho,” anasema

Kocha wa Simba (wakati huo), Patrick Phiri alimsimamisha Manyika langoni wakati mabeki walikuwa William Lucian, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka na Joseph Owino, wachezaji wengine ni Jonas Mkude, Haruna Chanongo na Said Ndemla. Pia alikuwapo Elias Maguli, Amri Kiemba na Emmanuel Okwi. Katika benchi alikuwapo Ivo Mapunda, Amisi Tambwe, Ramadhan Singano, Shabani Kisiga, Issa Rashid na Abdulaziz Makame.

Mechi hiyo ilikuwa na ushindani wa aina yake kutokana na presha za nje ya uwanja huku Yanga ikionekana kupewa nafasi zaidi ya kushinda kutokana na muunganiko waliokuwa nao, lakini Manyika alisimama imara. Licha ya mara kadhaa kupata kashikashi Mapunda alikuwa akisimama kama anapasha kuzuga.

Kipa huyo anasema kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa sasa kumekuwapo na ushindani mkubwa kutokana na wachezaji wengi kuwa na mzuka wa kutaka kufanya mambo makubwa na kutengeneza maisha yao ya ndani na nje ya uwanja.

Mchezaji huyo anaamini kwamba Polisi Tanzania itafanya vizuri zaidi msimu huu mara Ligi Kuu itakaporejea kwani wachezaji wake kila mmoja anajitambua na ana ari ya kupambana huku wakipata sapoti kubwa ya mashabiki wao.

Advertisement