Lusajo 'aiua' Azam, afikisha bao 10

BAO la mshambuliaji wa Namungo FC, Reliants Lusajo dhidi ya Azam FC, limeipandisha timu hiyo nafasi ya pili kwa kufikisha alama 43 katika mechi 23 walizocheza.
Endapo Yanga kesho Jumapili ikashinda dhidi ya Coastal Union itapanda hadi nafasi ya pili ikiwa imefikisha pointi 43 ambapo hadi leo Jumamosi ina pointi 40.
Lusajo aliipatia timu yake bao hilo la ushindi dakaika ya 60, ambaye alimchungulia kipa Razak Abalora aliyekuwa ametoka akapiga shuti kali lililoenda moja kwa moja nyavuni.
Lucas Kikoti alipiga pasi akiwa katikati ya uwanja, iliomkuta Lusajo ambaye akatumia akili ya kumsoma kipa kisha kupiga shuti, lililowaamsha mashabiki wao kushangilia timu hiyo.
Hilo linakuwa bao la 10 kwa Lusajo akiwa nyuma mabao matatu kwa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ambaye anaongoza mabao 13.
Dakika ya 68 Lusajo alijaribu kupiga shuti kali nje ya 18 na kama sio uhodari wa Abalora kupangua basi angefunga bao la pili.
Dakika ya 72 Blaise Bigirima alikosa bao la wazi akiwa amebakia na Abalora ambapo alichongewa pasi nzuri na Lusajo.
Kupatika bao dakika ya 60 kuliiamsha Namungo kucheza pasi zenye utulivu zilizokuwa zinafika langoni kwa Azam FC na kuwafanya mabeki, Bruce Kangwa, Yukub Mohamed na Agrey Morris ambao muda mwingi walijikuta wakipambana kudhibiti hatari zilizokuwa zinaelekezwa langoni kwao.
Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba alifanya mabadiliko dakika ya 75 alimtoa Obrey Chirwa akiingia Donald Ngoma aliyeonekana kuisumbua beki ya Namungo FC kutokana na kutumia nguvu.
Ngoma hakuonyesha uoga wa kuwafuata mabeki wa Namungo FC kwenda kushambulia kwenye lango lao, ingawa juhudi zao zilishindwa kuzaa matunda.
Mechi nyingine zilizochezwa jioni ya leo Jumamosi ni kati ya Mwadui FC ambayo imeshinda mabao 2-1 dhidi ya Mbao , Mbeya City imeshinda bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar wakati JKT Tanzania imemfunga Kagera Sugar bao 1-0 huku Polisi Tanzania ikiifunga Ruvu Shooting bao 3-1.