Lunyamila awashukia kina Yondani

Muktasari:

Staa wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema kama kuna safu inatakiwa kufanyia marekebisho ndani ya timu hiyo ni safu ya ulinzi aliyodaiwa inashindwa kulinda ushindi timu ikiwa mbele kwa mabao.

STAA wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema safu ya ulinzi ya timu hiyo iluiyopo chini ya Kelvin Yondani na Lamine Moro, inahitaji marekebisho zaidi, kutokana na timu kupata matokeo wanayoshindwa kuyalinda.
Alitolea mfano Yanga ilipocheza na Zesco ya Zambia  mechi ya Ligi ya Mabingwa iliyopigwa jijini Dar es Salaam, kwamba ilitangulia kuongoza bao lakini walishindwa kulilinda na wakasawazisha dakika za majeruhi.
Lunyamila alisema kwa upande wake anaona safu ya ushambuliaji inafanya kazi yake vyema ikishirikiana na viungo hivyo alimtaka kocha Mwinyi Zahera kuangalia upya safu ya ulinzi.
"Mechi kama mbili Yanga ndio ilikuwa inaongoza ya Zesco na ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania, tafsiri yake ni mabeki hawakufanya kazi yao kisawasawa," alisema winga huyo wa zamani aliyewahi kutamba na Biashara Shinyanga, Malindi, Simba na Taifa Stars.
"Kila sekta ina umuhimu wake ndani ya dakika 90, washambuliaji wanatakiwa kupambana kufunga, viungo wanatakiwa kuchezesha timu na mabeki kulinda timu, timu inaongozwa badae mnakuja kufungwa lazima sekta mojawapo inakuwa haijakaa sawa," alisema.
Alisema kadri ligi inavyoendelea ndivyo ugumu unavyoongezeka, hivyo aliwataka nyota wa kikosi hicho kuongeza umakini kwenye kazi yao ili kutengeneza mazingira ya ubingwa mapema.
"Mashabiki na wanachama wa Yanga akili yao inawaza ubingwa hivyo lazima kikosi kianze kuonyesha taswira hiyo mapema," alisema.