Luis Miquissone hatihati kuikosa Kariakoo Derby

MASHABIKI wa Simba wanatamba kwa sasa kufuatia nyota wao watano kuitwa timu zao za taifa, lakini jambo hilo linaweza kugeuka pigo kuelekea mechi yao ya watani wa jadi dhidi ya Yanga iliyopangwa kupigwa, Oktoba 18, kwenye Uwanja wa Mkapa.

Simba imejikuta kwenye hatihati ya kuwakosa baadhi ya nyota wake hasa Luis Miquissone aliyeitwa timu ya taifa ya Msumbiji kutokana na kubanwa na ratiba ya mechi za kimataifa za kirafiki ambazo timu za taifa zitacheza siku chache zijazo.

Changamoto ya usafiri na ratiba ya kambi kwa baadhi ya nchi hasa Msumbiji, ni wazi sasa zinaipasua kichwa Simba kuona ni kwa jinsi gani itapambana kuwapata wachezaji wake kwa wakati ili wajiandae dhidi ya Yanga.

Wachezaji watano wa Simba walioitwa katika vikosi vya timu za taifa ukimjumuisha na Luis ni Francis Kahata na Joash Onyango (Harambee Stars ya Kenya) pamoja na Clatous Chama na Larry Bwalya (Chipolopolo ya Zambia).

Kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka la duniani (Fifa), kuanzia Oktoba 5 hadi 13 ni muda wa mechi za kimataifa za mashindano au za kirafiki ambapo wachezaji wanatakiwa kuwa na timu zao za taifa. Katika muda huo, Msumbiji imepanga kuweka kambi Ureno kuanzia jana na huko itacheza mechi za kirafiki na Guinea Bissau na Angola. Msumbiji itaanza na Guinea Bissau, Oktoba 8 na siku tano baadaye itaumana na Angola. Kwa maana hiyo, Luis atakuwa na siku nne za kusafiri kutoka Ureno hadi hapa nchini kuungana na kikosi cha Simba.

Zambia itacheza mechi mbili dhidi ya Kenya na Afrika Kusini, Oktoba 10 na 11.

Ikumbukwe baadhi ya nchi hasa za Ulaya zimeweka masharti kadhaa kwa wasafiri wanaoingia na kutoka katika nchi zao, jambo ambalo linaweza kuwachelewesha baadhi ya wachezaji wa Simba kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo au wakaukosa, ingawa benchi la ufundi limetamba limejiandaa kisaikolojia kukabiliana na changamoto hiyo.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipoulizwa na Mwanaspoti alisema: “Kimsingi hii ni changamoto kubwa na sio tu kwa Luis, bali hata hao wachezaji wengine ingawa tunapambana kwa kadri ya uwezo wetu kuhakikisha wachezaji wetu wote tunawapata katika wakati muafaka baada ya kuzitumikia timu zao za Taifa, lakini kama imeshindikana, hakuna namna tutawatumia watakaokuwepo kwa sababu timu iko vizuri na ratiba haiwezi kubadilika.

“Hata hivyo, hili ni jambo ambalo linapaswa kutazamwa zaidi siku za usoni kwa sababu kalenda ya Fifa ilikuwa inajulikana, hivyo ratiba yetu ilipaswa kuipa nafasi na pengine ni vyema isingepangwa mechi za ligi kuchezwa ndani ya muda huo ili kuwapa fursa wachezaji kutumikia timu zao za taifa.

“Mfano sasa wengi wanatazama mechi ya Simba na Yanga tu, lakini kumbuka wachezaji wanatakiwa kujiunga na timu zao Oktoba 5, lakini sisi tuna mchezo Dodoma siku ya Oktoba 4. Nadhani ni vyema ratiba ya ligi ingezingatia hilo. Hata hivyo vyovyote itakavyokuwa, tuko tayari kwa ajili ya mchezo huo.”

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, Azam FC ina wachezaji wawili ambao wameitwa katika timu zao za Taifa ambao ni Obrey Chirwa (Zambia) na Yakubu Mohammed aliyeitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana wakati kwa upande wa Yanga hakuna hata mmoja.