Liverpool ni kufa au kupona kwa Napoli leo

Monday December 10 2018

 

Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amewaambia wachezaji wake kuwa leo wanapaswa kucheza kufa au kupona ili kukwepa kung’olewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Liverpool yenye pointi sita leo itawaalika vinara wa kundi C, Napoli yenye pointi tisa katika mechi ya mwisho ya makundi, timu hiyo ni lazima ishinde, huku ikiomba PSG yenye pointi nane ifungwe na Crvena Zvezda inayoburuza mkia.

“Mechi dhidi ya Napoli imebeba hatima yetu kama tutashinda tutaendelea lakini tukishindwa tunaweza kuaga mashindano yote, ikiwa PSG itaishinda Crvena Zvezda sisi tutaingia Kombe la Europa Ligi.

“Jumanne usiku utakuwa mtihani kwetu, hii ni mechi kubwa na muhimu kwa Liverpool, pengine kuliko mechi yoyote tuliyocheza kwa msimu huu, ni ushindi tu dhidi ya Napoli utakaobeba nafasi yetu katika Ligi ya Mabingwa,” alisema Klopp.

Mbali na Liverpool timu nyingine ya England yenye hatihati ya kusonga mbele ni Tottenham yenye pointi saba sawa na Inter Milan, timu hiyo ni lazima ishinde ugenini dhidi ya Barcelona ambayo imeshafuzu 16 bora kinyume cha hivyo itaangukia Europa Ligi.

Timu za Manchester United na Manchester City zenyewe zimefuzu hatua ya 16 bora zikiwa na mechi mkononi na sasa zinasubiri ratiba ya mtoano ipangwe zijue zitakutana na timu zipi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la soka Ulaya (Uefa) Droo ya 16 bora itapangwa Desemba 17, mwaka huu na mechi za kwanza zitachezwa kati ya February 12 na 13 na nyingine zitachezwa kati ya Februari 19/20. Wakati zile za marudiano zitachezwa Machi 5 na 6 na Machi 12 na 13 mwakani.

Advertisement