Liverpool, Manchester City zawagawa mashabiki Manchester United, Arsenal

Muktasari:

  • Mashabiki wa klabu mbalimbali katika Ligi Kuu England wamegawanyika kuhusu timu inayostahili kutwaa ubingwa kati ya Liverpool na Manchester City

London, England. Leo usiku Manchester United watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani kucheza na Manchester City katika mechi muhimu iliyokuwa inatoa taswira nzima ya ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Liverpool na Man City ndizo zinazochuana katika mbio za ubingwa huo na kabla ya mechi hiyo Liverpool walikuwa kileleni kwa tofauti ya pointi, lakini wakiwa mbele kwa mechi moja, hivyo walikuwa wakitamani Man United washinde mechi yao kuwasafishia njia kwenye kubeba ubingwa.

Lakini, sasa wakati mbio hizo zikiendelea, kumefanyika utafiti wa kuzihusisha timu za Top Six kupata maoni yao wanadhani ni timu gani wangependa ibebe ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kati ya Liverpool na Man United na majibu ya kura hizo ni kichekesho.

Unaambiwa hivi, mashabiki wa Man United, karibu asilimia 64 walipiga kura za kutaka Man City ibebe ubingwa huo mbele ya Liverpool bila ya kujali kwamba ni majirani wao na kelele zao huenda zikawanyima raha huko Manchester. Kwa maana hiyo ni asilimia 36 tu ya mashabiki wa Man United ndio wanaotaka Liverpool ibebe ubingwa.

Katika zoezi hilo, Tottenham asilimia 53 ya mashabiki wake wanataka Liverpool ibebe ubingwa huku asilimia 47 wakitaka Man City ndio wabebe ubingwa, kiwango sawa na Arsenal ambao asilimia 53 ya mashabiki wake wanataka Liverpool ichukue taji hilo.

Chelsea wao asilimia 47 imetaka Liverpool ndio wawe mabingwa, wakati asilimia 53 wameichagua Man City, huku Everton wakitoa asilimia 67 ya Man City kuwa mabingwa na asilimia 33 tu ndio wanaotaka Liverpool wabebe ubingwa huo.

Kwa mechi za usiku wa leo ligi hiyo sasa imebakiza mechi tatu tu kufika ukingoni na hapo itafahamika nani amebeba ubingwa katika vigogo hao wawili wanaochuana jino kwa jino.