Lipangile aitanguliza KMC kwa Mtibwa Sugar

Friday January 17 2020

 

By Mwandishi Wetu

Mabao mawili ya Sadalah Lipangile yameipeleka KMC mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaoendelea Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ikicheza kwa kiwango bora, KMC ilipata bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Lipangile kwa shuti kali akimalizia pasi nzuri ya Serge Nogues.
Baada ya bao hilo KMC iliongeza mashambulizi langoni kwa Mtibwa Sugar na Lipangile tena akawainua mashabiki wa KMC. Lipangile aligusa mpira ulimpita kipa Shaban Kado aliyekuwa ametoka kuuwahi na kugongana na beki wake Cassian Ponela.
KMC imecheza dakika 45 za Kwanza kwa kiwango bora kuliko Mtibwa Sugar huku wachezaji wake wakitumia nguvu katika kushambulia na hata kukaba hivyo, kuwaweka katika wakati mgumu.
Mtibwa ambao ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, wanaonekana kucheza taratibu huku safu yao ya kiungo inayoongozwa na Abdulhalim Humid na Ally Yusuph ikishindwa kuiunganisha timu hiyo na pasi zao nyingi kunaswa na wachezaji wa  KMC.
Pia washambuliaji wa Mtibwa Sugar licha ya kufika golini kwa KMC mara kwa mara, lakini wameshindwa kuwa watulivu na mashuti yao mengi kutoka nje.

Advertisement