Lionel Messi: Huu ndo mzigo wake

Saturday September 19 2020

 

LONDON, ENGLAND. NANI hataki kuwa bilionea? Yupo? Hawezi kuwepo. Hata hivyo si kila mtu anaweza kuwa bilionea. Hata wanasoka mastaa wanaolipwa mishahara kila wiki, si wote wanaofikia hatua ya kuwa mabilionea.

Lakini, wiki hii iliyomalizika, staa wa Barcelona aliongoza orodha ya wanamichezo wenye pesa ndefu kwenye orodha iliyotolewa na Forbes, baada ya kufikia kipato cha Dola 1 bilioni (Pauni 760 milioni). Hivyo, Messi anakuwa mwanasoka wa pili kufikia daraja hilo baada ya mpinzani wake wa siku zote, Cristiano Ronaldo. Messi miaka yake 16 ya kucheza soka la kiwango cha juu huko Barcelona imemfanya akaunti yake ya benki kunona huku ikinogeshwa zaidi na dili za mikataba ya kibiashara inayojumuisha hoteli na kampuni ya mavazi. Messi amepiga pesa na kuwa bilionea akiwa na umri wa miaka 33.

MSHAHARA MNONO

Majira haya ya kiangazi, Messi alitishia kuihama Barcelona kabla ya kubadili mawazo na kubaki Noy Camp kwa mwaka mwingine zaidi ili kuendelea kuvuna mshahara mnono. Wakati Messi anainukia na kuwa staa wa Barca, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 20, alipewa mkataba uliokuwa na thamani ya Pauni 90,000 kwa wiki, mkwanja uliomfanya awe mmoja wa mastaa waliolipwa pesa ndefu. Hadi kufikia sasa, akiwa amebeba mataji 10 ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne, Messi mshahara wake umeongezeka maradufu - ambapo kwa mwaka anaingiza Pauni 71 milioni, hapo bila ya kujumuisha bonasi. Kutoka sasa hadi 2021, Messi akicheza asilimia 60, ataingiza kipato cha Pauni 98 milioni.

Kama ataisaidia Barca kubeba mataji matatu, akibeba Ballon d’Or tena, basi kwa mwaka anavuna Pauni 110 milioni.

Huu ni mwaka wake wa mwisho Nou Camp na kama atapata dili matata basi anaweza kuhama kutafuta malisho mapya.

Advertisement

DILI ZA UDHAMINI

Staa Messi amevutia makampuni kibao na kumdhamini kwa pochi nene. Kitendo cha kuwa na mashabiki wengi wanaomfuatilia, limemfanya staa huyo awindwe na kampuni kibao zinazotaka kumdhamini. Kwa mujibu wa Forbes, Messi anaingiza Pauni 24 milioni kwa mwaka kupitia dili hizo za kibiashara. Dili lake kubwa zaidi ni lile la Adidas alilosaini mwaka 2017, ambapo kwa mwaka linamwingizia Pauni 9 milioni.

Kampuni hiyo ya mavazi ya kimichezo, mwaka 2015 iliamua kabisa kutengeneza bidhaa yao maalumu kwa staa huyo, ilipotengeneza kiati kilichofahamika kama Adidas Messi. Hata Messi atakapostaafu soka, bado anatakuwa anaweka mfukoni mkwanja mrefu kama ilivyo kwa Air Jordan ambapo Nike ilitengeneza kwa ajili ya gwiji wa mpira wa kikapu, Michael Jordan. Kampuni nyingine za udhamini zinazomdhamini Messi kwa pesa ndefu ni Pepsi, Gatorade, Huawei, Budweiser na Mastercard.

MITINDO NA MAVAZI

Mwaka jana, Messi aliingia kwenye ulimwengu wa mitindo ya mavazi. Alitambulisha lebo yake ya mavazi, akishirikiana na Ginny Hilfiger na mavazi hayo yanauzwa kwenye maduka ya staa huyo, The Messi Store. Nguo zake ni bei mbaya. Fundi wa kampuni ya Bespoke Saville Row, Richard James naye amekuwa akishirikiana na Messi kwenye kushona suti na kuziweka kwenye maduka.

Maria Sol, dada yake Messi, anaripotiwa ndiye anayesimamia kwa kiasi kikubwa kukua kwa kampuni hiyo ya mitindo ya mavazi ya staa huyo wa kimataifa wa Argentina.

BIASHARA YA HOTELI

Mwaka 2017, Messi aliingia kwenye biashara ya hoteli baada ya kuinunua MiM Sitges iliyopo kwenye pwani ya Barcelona. Alitumia Pauni 26 milioni kununua hoteli hiyo ya nyota nne, ambapo juu kabisa kwenye paa kuna mgahawa, baa na bwawa na kuogelea, huku hoteli yenyewe ikiwa na vyumba 77 na gharama ya kulala hapo ni Pauni 120 kwa usiku mmoja. Hoteli hiyo ipo karibu kabisa ya ufukwe.

Hivi karibuni, Messi aliripotiwa kununua hoteli pia Majorca na Ibiza, akiwekeza kwenye biashara hiyo, ambayo itamfanya staa huyo kuendelea kuingiza tu kipato hata atakapostaafu soka. Kwa miradi yake hiyo, Messi ataendelea kuwa tajiri hata kama ataacha soka.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisement