Ligi Kuu Bara yaanza bila Simba, Yanga

Muktasari:

Staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella amesema zama zimebadilika akidai kwenye kazi ya kupanga ratiba ina watalamu ambao wameona ni vyema ligi ikaanza nje ya Simba, Yanga na Azam FC.

LIGI kuu Bara inaanza rasmi jioni ya leo, lakini vigogo Simba, Yanga na Azam FC hazipo kwa vile zina majukumu yao kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kitendo cha timu hizo kukosekana zimefanya wadau kukiri kwamba mambo kwa sasa yamebadilika na haishangazi sana kuona vigogo wakiwa nje ya ufunguzi wa msimu mpya.
Staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella amesema zama zimebadilika akidai kwenye kazi ya kupanga ratiba ina watalamu ambao wameona ni vyema ligi ikaanza nje ya Simba, Yanga na Azam FC.
"Nyakati zimebadilika sana, tangu nianze kucheza ama mpaka sasa sikumbuki kama imewahi kuanza ligi kuu Bara Simba na Yanga zote zikakosa kufungua pazia"
"Lakini tunapaswa kuheshimu kila kinachofanywa na wale ambao wapo kwenye sekta za kupanga ratiba, ingawa zikicheza hizo timu kunakuwa na amsha amsha ya mashabiki kujua timu zao zimewaletea nini kwa msimu mpya," amesema.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa KMC, Mrage Kabange amesema wanatakiwa kuendana na ratiba ya ligi kuu inavyowaongoza bila kuangalia Simba, Yanga na Azam FC kutofungua pazia la msimu mpya.
"Hata sisi ndio maana tutacheza Jumanne na Azam FC kwa sababu tulikuwa kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ndio maana hatutaanza leo Jumamosi, hatuna budu kuzingatia ratiba inavyoelekeza," amesema.