Ligi Daraja la Kwanza shughuli bado mbichi

Tuesday June 30 2020
FDL PIC

BAADA ya wikiendi kumalizika kwa mzunguko wa 20 huku Gwambina FC ikiwa timu ya kwanza kupanda Ligi Kuu, kazi imekuwa ngumu kwa timu zilizosalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Miamba miwili inayoongoza kundi A, Dodoma Jiji FC na Ihefu bado inatafutana baada ya wiki iliyopita kucheza ugenini na kufanikiwa kuvuna alama tatu.
Ihefu iliilaza African Lyon kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati Dodoma Jiji iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Majimaji mkoani Ruvuma 
Wiki hii Dodoma Jiji itakipiga na Mbeya Kwanza inayosaka nafasi ya kucheza hatua ya mtoano na Ihefu itaikaribisha Friends Rangers.
Dodoma Jiji inasaka alama tatu ili kuzidi kubaki kileleni wakati Mbeya Kwanza ikimkimbia Majimaji ambayo imelingana naye alama zote zikiwa na pointi 37 kila moja.
Kocha wa Mbeya Kwanza, Michael Mnyali anasema ushindi ndio jambo ambalo wanalifuata Dodoma ili kuzidi kufufua matumaini ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Maka Mwalwisi kocha wa Ihefu FC anasema ni kipindi kigumu kwa timu zote za kundi hilo kutokana na ushindani ulivyo na kulifanya kila timu kuingia uwanjani kwa tahadhari kubwa.
"Huu ndio wakati wa makocha kujua hali ya vikosi vyao baada ya michezo kuchezwa. Upande wetu tunaendelea kujiimarisha kila kukicha maana ligi inamalizika ikiwa na ushindani mkubwa," alisema Mwalwisi.
Vita nyingine ipo Kundi B kwa timu ya Geita Gold inayoshika nafasi ya pili kwa alama 34, Gipco FC na Transit Camp zenye alama 29 na AFC yenye alama 28 ambayo ipo nafasi ya tano.
Timu zote bado zina nafasi ya kupambana katika michezo miwili iliyobaki na kutinga hatua ya mtoano.
Kwa timu zinazoshuka daraja, kundi A tayari Green Warriors imeshashuka, huku Mlale FC na Pan African zikiwa tayari zimeaga rasmi ligi hiyo kwa upande wa kundi B.

Advertisement