Libya pia wako ugenini, Stars twende Afcon

Muktasari:

Kufungwa 4-1 dhidi ya Tunisia katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi J la kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021, hakumaanishi kuwa Libya ni timu mbovu ya kutupa kujiamini sana tutakapokutana nao leo

KAMA chati ya viwango vya ubora wa soka duniani inayotolewa na Fifa ingekuwa inaamua mshindi wa mechi, pasingekuwa na haja ya baadhi ya mechi kuchezwa.

Lakini soka haliko hivyo. Ndiyo maana ni mchezo unaopendwa zaidi duniani kutokana na matokeo yanayosubiri hadi mechi ichezwe. Matokeo ya kwenye makaratasi ni tofauti kabisa na kinachotokea uwanjani.

Kwa mujibu wa viwango vya Fifa, Libya inashika nafasi ya 103 duniani katika ubora wa soka wakati Tanzania sasa inashika nafasi ya 133. Hii inamaanisha kwamba Libya wako vizuri zaidi yetu.

Lakini hilo halitufanyi tuwaogope Libya, japo ni muhimu kuwaheshimu kwa ubora wao.

Kufungwa 4-1 dhidi ya Tunisia katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi J la kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021, hakumaanishi kuwa Libya ni timu mbovu ya kutupa kujiamini sana tutakapokutana nao leo.

Tunisia ni timu inayotisha kwa hivi sasa barani Afrika ikishika nafasi ya pili kwa ubora nyuma ya Senegal inayoshika nafasi ya 20 duniani. Tunisia ni ya 29 kwa ubora wa soka duniani.

Hivyo Tunisia kuifunga Libya magoli 4-1 si jambo la kushangaza, japo si lazima timu iliyo juu katika viwango kuifunga ya chini.

Kwa vile kuwa katika nafasi za juu za ubora wa soka hakuihakikishii timu ushindi, ndiyo sababu Stars ikaizamisha Guinea ya Ikweta 2-1 katika mechi yao ya awali ya kufuzu Afcon 2021 Ijumaa iliyopita, licha kwamba wapinzani wetu hao wanashika nafasi ya 78 duniani.

Katika mechi ya leo, Watanzania hatupaswi kujiona tuko ugenini, kwa sababu hata Libya nao wako ugenini. Mechi hiyo inachezwa Tunisia kutokana na wasiwasi wa hali ya usalama nchini Libya.

Tunayo kila sababu ya kuwaendesha puta na kuwafunga wapinzani wetu hao leo.

Rekodi dhidi yao inaonyesha tumekutana nao mara moja tu Desemba 3, 2017 katika mechi ya Kombe la Cecafa na tukatoka nao 0-0. Hii ina maana kwamba hatuna tofauti nao kubwa katika soka uwanjani licha ya kwamba wametupita mbali katika viwango vya Fifa.

Tukikomaa tukawafunga Walibya leo itakuwa ni kujiweka vyema katika kuwania nafasi mbili za kufuzu kwenda Afcon 2021.

Fainali za 33 za Afcon zitakazofanyika nchini Cameroon, zitahusisha mataifa 24 kutoka katika timu 48 zinazochuana sasa katika makundi 12 yenye timu nne-nne. Timu mbili kutoka katika kila kundi zitafuzu, jambo linalomaamisha kwamba nusu ya mataifa yanayochuana katika hatua hii ya makundi, yataenda Cameroon 2021.

Tanzania imekuwa na mafanikio katika miaka ya karibuni na hii inachangia hamasa ya kutaka tufuzu tena Afcon.

Baada ya kusotea kwa miaka 39 tangu ilipofuzu kwa mara kwanza Afcon 1980, Tanzania ilitisha iliposhiriki fainali zake za pili za Mataifa ya Afrika mwaka huu nchini Misri na pia Stars imefuzu kwa mara ya pili fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji za ligi za ndani (Chan) 2020 itakayofanyika pia Cameroon.

Matokeo haya yanathibitisha kuwa uwezo tunao na nia tunayo. Twendeni tena Afcon 2021.