Lampard mayai viza yanamsubiri miezi 6 tu

Muktasari:

Lakini pia anaamini kwamba mashabiki waChelsea watamvumilia kwa nusu msimu tu kama mambo hayataenda vyema.

LONDON, ENGLAND.KOCHA mpya wa Chelsea, Frank Lampard, ameonywa na beki wa timu hiyo, David Luiz kwamba mashabiki watamvumilia kwa miezi sita tu kabla ya kuanza kutarajia mafanikio.
Gwiji wa Chelsea, Lampard amerejea klabuni hapo akiwa kocha kuchukua nafasi ya Maurizio Sarri baada ya Muitalia huyo kutimkia Juventus.
Katika kufanya hali ngumu kwa Lampard na Chelsea, klabu hiyo imefungiwa kusajili wachezaji wapya jambo linalowalazimu kuwaamini makinda wao wa akademi huku pia wakiuza jembe lao Eden Hazard kwa Real Madrid.
Kutokana na mazingira hayo na jinsi mashabiki wanavyomkubali Lampard, David Luiz anatarajia kuona kocha huyo mpya akivumiliwa zaidi ya waliomtangulia.
Lakini pia anaamini kwamba mashabiki waChelsea watamvumilia kwa nusu msimu tu kama mambo hayataenda vyema.
"Nadhani kila mmoja anaelewa hali ilivyo na anatambua anatakiwa kuwa mtulivu," beki kitasa huyo alisema.

"Watavumilia kwa miezi sita tu na kisha katika miezi sita itakayofuata ya msimu watataka tushinde.

"Itakuwa hivyo, tunapaswa tulifikirie hilo na tutafute njia sahihi ya kuwapa furaha.

"Kama haufikiri kwa mtazamo huo (kuhusu kutwaa makombe), basi huwezi kuichezea Chelsea. Dhamira inapaswa kuwa juu. Hakika kuna timu nyingi zinazotisha.”
Aliongeza: "Nadhani tumempoteza mchezaji mkubwa sana na gwiji klabuni Chelsea, Eden Hazard, lakini tunao wachezaji wengi wa kufanya kazi yake."