Lampard amwagia mkwanja Abramovich

Muktasari:

Mastaa 21 wameondoka Chelsea, akiwamo supastaa wao Eden Hazard na straika Alvaro Morata, jambo lililomfanya Lampard awe ameingiza klabuni mkwanja wa Pauni 173 milioni.

LONDON, ENGLAND.FRANK Lampard hana hata mwaka kwenye klabu ya Chelsea tangu awe kocha, lakini hadi sasa tayari ameshampa faida ya mkwanja mrefu mmiliki Roman Abramovich kuliko makocha wengine wote waliomtangulia Stamford Bridge.
Lampard ameifanya The Blues kuandikisha faida ya Pauni 133 milioni kutokana na mauzo ya wachezaji kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, lililofungwa rasmi Jumatatu iliyopita.
Kocha huyo hakuwa na uwezo wa kusajili mastaa wapya baada ya kutua Stamford Bridge akitokea Derby na hiyo ni kwa sababu Chelsea imefungiwa kusajili.
Mastaa 21 wameondoka Chelsea, akiwamo supastaa wao Eden Hazard na straika Alvaro Morata, jambo lililomfanya Lampard awe ameingiza klabuni mkwanja wa Pauni 173 milioni.

Lakini kiwango hicho kimepungua na kubaki faida ya Pauni 133 milioni, kwa sababu alitoa Pauni 40 milioni kumbakiza Mateo Kovacic Stamford Bridge kwa sababu alikuwa akirudi Real Madrid baada ya mkataba wake kumalizika.
Kocha mwingine aliyewahi kumwingiza faida Abramovich kwenye kipindi cha usajili ni Mbrazili, Felipe Luiz Scolari, lakini faina yenyewe ilikuwa Pauni 13 milioni tu mwaka 2008, wakati alipowanasa Jose Bosingwa na Deco huku akiwafungulia mlango wa kutokea mastaa kibao akiwamo Shaun Wright-Phillips na Wayne Bridge waliokwenda Man City.
Makocha wengine waliopita, Claudio Ranieri alitumia Pauni 152 milioni, aliingiza Pauni 1 milioni, hasara ikawa Pauni 151 milioni. Mourinho alitumia Pauni 150 milioni, akatengeneza Pauni 3 milioni, hasara ikawa Pauni 147 katika msimu wa kwanza (2004/05) na misimu mingine yote iliyofuatia, alitia hasara tu kwenye kipindi cha usajili, hata aliporudi kwenye kikosi hicho kwa mara ya pili.
Carlo Ancelotti alitia hasara ya Pauni 118 milioni, wakati Maurizio Sarri aliweka hasara ya Pauni 124 milioni. Andre Villas-Boas alitia hasara ya Pauni 58 milioni, Roberto Di Matteo na Antonio Conte waliweka hasara ya Pauni 76 milioni na Pauniu 75milioni mtawalia.
Kocha Conte ndiye aliyetumia pesa nyingi kusajili kuliko wengine wote, Pauni 234 milioni, lakini kwa makocha wote waliopita Stamford Bridge chini ya Abramovich, kwenye usajili wametia hasara ya Pauni 744 milioni.