Lampard amtabiria makubwa kinda wake

Muktasari:

Mara ya mwisho kwa Tammy Abraham kuifungia bao Chelsea ilikuwa ni Januari 11 na baada ya hapo akapoteza nafasi mbele ya Olivier Giroud

London,England. Kocha wa Chelsea, Frank Lampard anaamini kuwa hali ya kujiamini kwa mshambuliaji wake Tammy Abraham itarejea baada ya kinda huyo kufunga bao la ushindi dhidi ya Crystal Palace jana kwenye Ligi Kuu ya England.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, kabla ya bao hilo lililoipa Chelsea, ushindi wa ugenini wa mabao 3-2, hakuwa amefunga bao lolote tangu Januari alipofunga dhidi ya Burnley.

Lampard alisema ana imani bao hilo litasaidia kurudisha makali ya Abraham ambaye katika siku za hivi karibuni amejikuta akipoteza nafasi mbele ya Olivier Giroud.

"Ni bao muhimu kwa Tammy ambaye amecheza kwa muda mrefu bila ya kufunga. Litaongeza hali yake ya kujiamini, ni kitu kizuri kwangu, nitakuwa na chaguo lingine.

Aliingia dakika za mwisho na akafunga bao la ushindi nimemfurahia mshambuliaji wangu," alisema Lampard.

Katika mchezo huo, Chelsea walilazimika kufanya kazi ya ziada kupata ushindi mbele ya Crystal Palace waliokuwa wasumbufu katika uwanja wao wa Selhurst Park.

Baada ya kutangulia kwa mabao matatu yaliyopachikwa na Olivier Giroud, Christian Pulisic na Abraham, Chelsea ililazimika kuwa kwenye presha kubwa baada ya Palace kupata mabao yake mawili kupitia kwa Wilfried Zaha na Christian Benteke.

Palace walifanya idadi kubwa ya mashambulizi katika dakika za lala salama na ilikuwa ni kama bahati tu iliyowabeba Chelsea kutopoteza pointi katika mchezo huo jambo ambalo hata Lampard amelikiri.

"Kepa (Arrizabalaga) alituokoa, Kurt (Zouma) naye aliokoa kwa kulala vizuri. Hizo zilikuwa dakika za hatari kwetu," alisema kocha huyo.

Ushindi huo unaifanya Chelsea kujiweka pazuri katika harakati zao za kupigania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao lakini pia sare ya mchezo kati ya Leicester City dhidi ya Arsenal, inaifanya 'The Blues' kuwa nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 60.

Chelsea wanatarajia kuwa ugenini katika mchezo ujao dhidi ya Sheffield United, Jumamosi na baada ya hapo watarejea nyumbani ambako wataikaribisha Norwich City