Lampard amlaumu Zouma badala ya Kepa

London, England. Kocha Frank Lampard amemtetea kipa wake, Kepa Arrizabalaga huku akisisitiza kuwa pasi ya Kurt Zouma kwenda kwa kipa huyo ilikuwa fupi.

Chelsea ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge juzi, wakati wakati kosa la ulinzi likiwagharimu dhidi ya Southampton.

Zouma alitaka kupiga pasi ya nyuma, lakini badala yake, Che Adams aliwahi na kufunga.

Kipa huyo wa kimataifa wa Hispania, Kepa alionekana kusita kucheza mpira huona badala yake akagongana na mshambuliaji.

Adams alifanikiwa kuuwahi mpira, aligeuka na kufunga kwa shuti kufanya matokeo kuwa 2-2.

Licha ya tukio hilo, Lampard alimtia lawamani Zouma kuwa alisababisha tatizo hilo kwa pasi yake fupi kwa Kepa.

Lampard alisema: “Sikuangalia tena tukio lile, nililiona moja kwa moja uwanjani.

“Pasi ilikuwa fupi na Kepa alilazimika kutoka kujaribu kuzuia.

“Na kama mnavyojua, hiyo ni bahati nasibu kwa hali ikiwa hivyo.

“Sikuona zaidi ya hapo, lakini kiukweli lilikuwa goli la kuudhi kwa upande wetu.”

Kipa huyo aliyenunuliwa kwa rekodi ya dunia, Kepa alinunuliwa kutoka Athletico Bilbao kwa Pauni 71.6 milioni 2018, alianza golini kutokana na kipa Edouard Mendy kuumia.

Aliruhusu mabao matatu, wakati Chelsea ikipoteza uongozi katika michezo ya sare ya mabao 3-3.

Timo Werner alifunga mabao mawili kipindi cha kwanza, kabla ya Danny Ings kusawazisha moja. Baada ya Adams kufunga, Havertz alifunga la tatu kwa Chelsea.