Lampard aahidi kumlinda Silva

London, England. Kocha Frank Lampard amepanga kumtumia kwa tahadhari beki mkongwe, Thiago Silva baada ya mchezaji huyo kuonyesha kiwango bora dhidi ya Sevilla juzi usiku.

Wakati Chelsea ikitoka katika matatizo ya safu ya ulinzi dhidi ya Southampton, alipoporwa ushindi dakika za mwisho, Silva alirudi kikosini na kuonyesha uzoefu kwa kutoruhusu bao kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Akiwa na miaka 36, Lampard anajua kuwa Silva anatakiwa kutumika kwa uangalifu kutokana na umri wake na kutochezeshwa katika kila mchezo, huku akikiri kuwa kuna tofauti katika kila mchezo ambao Chelsea inacheza bila beki huyo.

“Nadhani alikuwa bora zaidi leo,” alisema Lampard. “Nilizungumza kuhusu ubora na yzoefu kabla ya mchezona bahati nzuri amefanya vyote na alikuwa na mchezo mzuri.

“Ana uwezo mkubwa hasa katika suala la kutoruhusu kufungwa. Zaidi ya msimu, nitajaribu kumlinda na uzuri ni kwamba nina ukaribu naye licha ya kutumia mkalimani.

“Siku zote nafanya kazi pamoja naye na nakumbuka nilikuwa pia katika umri kama wake wakati wa msimu wangu wa mwisho wa Ligi Kuu England.

“Hivyo nitakuwa makini zaidi katika kumlinda na upangaji wangu wa kikosi, tunamhitaji zaidi.”

Chelsea imecheza mechi tatu bila kuruhusu bao msimu huu, dhidi ya Barnsley, Crystal Palace na Sevilla na Silva ameshiriki katika michezo hiyo yote ya mafanikio ya kutoruhusu bao.