Lallana rasmi atua Brighton

Muktasari:

Lallana amejiunga na Brighton akiwa ametoka kutwaa mataji mawili makubwa akiwa na majogoo wa jiji  Liverpool ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita wa 2018/19 huku msimu huu 2019/20  ikiwa ni Ligi Kuu England.

London, England. Brighton wamethibitisha kumsajili kiungo kutoka Liverpool, Adam Lallana kwa mkataba wa miaka mitatu.

Nyota huyo wa zamani wa Southampton alifanyiwa vipimo wiki hii lakini usajili wake unaelezwa ulikamilika mapema na ilibidi Brighton wasubiri hadi atakapomaliza sherehe za kusheherekea ubingwa aliotwaa wa Ligi Kuu England.

Lallana amekuwa mchezaji wa pili wa Liverpool kuondoka Anfield baada ya msimu kumalizika wa kwanza ni beki Dejan Lovren ambaye amejiunga na miamba ya soka la Russia, Zenit St Petersburg.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na Brighton, Lallana amesema anajiona kufanya maamuzi sahihi huku akidai haikuwa rahisi kufanya uchaguzi wa kujiunga na timu hiyo.

"Ninasubiri kwa hamu kuvuta hewa mpya nikiwa hapa. Vipimo vyangu vya afya vimeenda vizuri, kila kitu ni kipya na natazama mbele kukabiliana na changamoto mpya na nipo tayari.

"Miundo mbinu ambayo imeizunguka Brighton imenivutia, kuna wachezaji wengi wenye umri mdogo na vipaji na uwezo mkubwa," amesema kiungo huyo

Upande wa kocha wake mpya, Graham Potter amesema kufanya kazi na kiungo huyo ni jambo jema na kusisitiza kuwa hakuna mtu mwenye shaka  juu ya uwezo wake.

"Ni mchezaji wa daraja la juu katika ngazi zote kuanzia klabu hadi timu ya taifa," amesema.