Labda kama Neville anaamini uchawi na nuksi

Saturday August 17 2019

 

UNAAMINI kwamba wachambuzi wa Tanzania ni mashabiki wanazi? Msikilize Gary Neville. Namkubali. Ni mchambuzi mahiri lakini kuna wakati anachomekea unazi wake huku akiwa amekunja sura. Unaweza kudhani anaongea kwa masihara kumbe anakiamini anachoongea.

Majuzi alisikika akidai anaamini Manchester United itachukua ubingwa wa England kabla ya Liverpool. Aliyasema hayo bila ya soni mbele ya staa mwenzake wa zamani wa England, Jamie Carragher ambaye ni mchezaji wa zamani wa Liverpool na mnazi wa Liverpool.

Neville anaamini anachokisema? Sijui. Labda kwa sababu ni mzaliwa wa Bury, Manchester. United ni timu nzuri lakini Liverpool na Manchester City ni moto wa kuotea mbali kwa sasa. Hatuna hata uhakika kama United atatinga Top Four msimu ujao. Lakini swali hili lilishaondoka Liverpool kwa miaka kadhaa sasa. Swali lao ni kama wanaweza kuchukua ubingwa.

Neville anasema haya wakati Liverpool hii iliyotimia kila idara msimu uliopita ilifikisha pointi 97 na kukosa ubingwa wa England. Sir Alex Ferguson licha ya kuchukua mataji lukuki ya Ligi Kuu ya England hakuwahi kutwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 97.

Hii ina maana msimu uliopita Liverpool iliukosa ubingwa kwa sababu ya Pep Guardiola tu lakini ilishafikia pointi za ubingwa.

Kama Neville anaamini katika uchawi au nuksi naweza kumuamini lakini kama ni hali halisi, basi Manchester United na rafiki zao wa zamani waliotawala Ligi Kuu ya England, Arsenal bado wana hatua kadhaa za kuchukua ubingwa wa England. Lakini kama Liverpool ikichukua ubingwa hakuna atakayeshangaa. Kila timu ina ndoto ya kuwa na Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino. Lakini sio kila timu ina ndoto ya kuwa na Anthony Martial, Marcus Rashford na Jesse Lingard. Ukweli zaidi ni kwamba kuna mchezaji mmoja au wawili wa United wanaoweza kupata nafasi kikosi cha Anfield. Niliitazama sura ya Neville wakati anaongea hayo. Nilitamani kuona akitabasamu au kucheka kuashiria alikuwa anafanya masihara lakini kadri alivyoikunja sura yake nikajua alikuwa hatanii. Hapo ndipo nilipojishawishi kwamba labda Neville anaamini katika ushirikina au nuksi. Lakini kwa kile tunachokiona uwanjani, United ipo maili nyingi nyuma ya vijana wa Anflied.

Advertisement

Advertisement