Kwasi aamua kulianzisha mapema Simba

Muktasari:

  • Kauli ya Kwasi kuamua kuanza mazoezi na kikosi cha Simba, imekuja huku mabosi wa klabu yake ya zamani, wakiendelea kusisitiza kuwa Mghana huyo bado ni mali yao na wataishangaa sana Simba kama itaamua kumtumia sasa.

KITASA kipya cha timu ya Simba, Asante Kwasi, ameamua kulianzisha. Beki huyo aliyenyakuliwa kutoka Lipuli amesisitiza kuwa anajitambua kama mali ya Simba na kwamba asubuhi ya leo Jumatatu ataliamsha dude na wenzake katika mazoezi ya timu hiyo ndani ya kambi ya Polisi, jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Kwasi kuamua kuanza mazoezi na kikosi cha Simba, imekuja huku mabosi wa klabu yake ya zamani, wakiendelea kusisitiza kuwa Mghana huyo bado ni mali yao na wataishangaa sana Simba kama itaamua kumtumia sasa.

MSIKIE MGHANA

Beki huyo wa kati anayekaba mpaka kivuli, aliliambia Mwanaspoti kuwa yeye ni mchezaji wa Simba baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na suala linalolalamikiwa na viongozi wa Lipuli lilishamalizwa na meneja wake.

Kwasi alisema yeye ni mchezaji aliyekuja nchini kusaka maisha, hivyo pale inapotokea nafasi nzuri hawezi kuipotezea na kwamba leo atatimba kwenye mazoezi ya Wekundu wa Msimbazi yanayofanyika Chuo cha Polisi, Kurasini.

Alisisitiza aliamua kusaini Simba kwa kutambua atapata fursa ya kucheza soka la kimataifa kwani kikosi hicho kitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

“Nimesaini Simba na nitakuwa hapa kuanzia sasa kwa mechi zilizosalia za Ligi Kuu na kuhusu Lipuli, nina imani Meneja wangu atakuwa ameshamalizana kila kitu, ila niseme wazi kilichonisukuma kusaini Msimbazi ni kutaka kucheza mechi za kimataifa mwakani,” alisema Kwasi alipotafutwa jana kwa simu.

LIPULI WABISHI

Hata hivyo uongozi wa Lipuli kupitia Meneja, Mrisho Gambo, umesema wanachotambua ni kwamba Kwasi bado ni mchezaji wao na yupo katika orodha ya wachezaji watakaoendelea kuichezea Lipuli katika Ligi Kuu Bara.

Gambo alisema baada ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu wametangaza majina ya wachezaji waliowasajili na kuwatema na hakuna kokote walipoweka jina la Kwasi kuwa ameachwa. hivyo wanaishangaa Simba.

“Kwasi bado ni mchezaji wetu, ana mkataba na Lipuli utakaomalizika mwisho wa msimu, hivyo suala la kusajiliwa na Simba, mimi sijaambiwa lolote na wala sijui kama atakuwa na timu hiyo katika mzunguko wa pili,” alisema Gambo.

“Wachezaji wote wa kigeni na wazawa wameripoti kambini kwa maandalizi ya mechi ya Kombe la FA na Ligi Kuu na hata Kwasi anatakiwa kuripoti kambini kama walivyofanya wengine wote, jina lake bado lipo katika orodha ya nyota wetu,” alisema Gambo.

SIMBA KUFUNGUKA

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alipoulizwa juu ya ishu ya Kwasi na msimamo wa mabosi wenzao wa Lipuli, alisema kwa kifupi kuwa mambo yote ya usajili wa klabu yao utawekwa hadharani muda wowote wiki hii.

“Juu ya usajili na mambo mengine ya Simba tutayaweka hadharani katika mkutano na wanahabari nitakaouitisha, hivyo vuta subira,” alisema Manara.

Kikosi cha Simba kikiwa kamili baada ya nyota wake wa kigeni na wale waliokuwa timu ya taifa kuwasili, kitaendelea na mazoezi yao leo Chuo cha Polisi kujiandaa na mechi yao ya Kombe la FA na zile za Kombe la Mapinduzi na Ligi Kuu Bara kabla ya mwakani kuanza kibarua anga za kimataifa.

Mbali ya Kwasi, mchezaji mwingine mpya anayetarajiwa kuonekana kwenye mazoezi hayo ya Wana Msimbazi ni straika kutoka Msumbiji, Dayo Domingos Antonio.