Kwa vituko hapa ndio nyumbani

Muktasari:

  • Wapo wachezaji waliofanya vioja ambavyo kila pakizungumzwa visa na mikasa katika soka lazima majina yao yawemo katika orodha ya viumbe waliotia fora.

Tangu zama za kale mchezo wa kandanda umekuwa na viumbe wenye vituko unavyoweza kuvitengezea mchezo wa sinema na kuwa burudani nzuri kuliko mchezo unaokwenda dakika za nyongeza na kumalizia kwa kupigiana matuta ili apatikane mshindi.

Wapo wachezaji waliofanya vioja ambavyo kila pakizungumzwa visa na mikasa katika soka lazima majina yao yawemo katika orodha ya viumbe waliotia fora.

JOSE LUIS CHILAVERT

Mmoja wao ni golikipa na nahodha wa zamani wa Paraguay, Jose Luis Chilavert. Katika mwaka 2000 Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (FIFA) lilipowauliza waamuzi wa kimataifa mchezaji gani walimwona machachari na hatabiriki, wengi wao walimtaja Chilavert.

Mchezaji huyu ni mwenye hasira, mdomo wake umejaa kauli chafu zisioelezeka na mara nyingi alipigana makonde ndani na nje ya uwanja.

Paraguay ilipocheza nyumbani au nje ya nchi zaidi ya robo ya watazamaji walikwenda kuangalia mchezo ili kuona vituko vyake.

Alitumia miguu yote miwili na ipo siku alipokuwa akitaka kupiga penalti alimuuliza mwamuzi kama angeweza kutumia mkono au kichwa. Siku moja alipoulizwa mguu wake upi ulikuwa na mashuti makali zaidi alisema waliofaa kulijibu swali hilo ni magolikipa aliowasukumia makombora.

Kati ya mabao 62 aliyofunga akiwa golikipa moja ni la masafa ya mita 50 alilomfunga golikipa wa River Plate ya Argentina, German Burgos, katika mchezo wa ligi akiwa anaichezea Velez Sarsfield. Bao hili limetengenezewa filamu ya video. Siku moja alifunga penalti zote tatu walizopewa Paraguay katika mchezo, mbili kwa mguu wa kushoto na moja kwa mguu wa kulia.

Golikipa huyu mwenye majina mengi, Mbabe, Nyati, Mbwa na El Chila (nahodha jabari), mara nyingi aliingia katika migogoro ndani na nje ya uwanja.

Kwake yeye ni kawaida kuwachapa makonde waandishi wa habari, kuwatemea mate wachezaji na waamuzi na kuwapiga magolikipa, wachezaji wenzake na watazamaji. Kauli yake maarufu ni …Dawa ya mkorofi ni makonde tu.

Katika mwaka 1999 alisusia mashindano ya Copa Amerika kwa kusema aliona uchungu kwa serikali ya dikteta Rais Nicanor Duarte imetumia mamilioni ya Dola kuandaa mashindano wakati wananchi walikuwa na maisha magumu. Alipofungwa jela mashabiki wa kandanda wa Paraguay walikuja juu na kusema kama Chilavert hakutolewa na wao wangelikwenda kuishi jela. Madikteta walilazimika kumtoa jela.

Viongozi wa Fifa walipomtaka asitumie matusi aliwaambia: “Shikeni adabu zenu, kumbukeni mnafurahia mvinyo wakati wanaowapatia fedha za kufanya hivyo kwa kulipia kuingia viwanjani wanakufa njaa.” Siku moja aliwaudhi watu wa Australia aliposema wachezaji wengi wa nchi hiyo ni mashoga na ndio maana unapowapiga chenga walikuwa wanakukumbatia. Alifungiwa na Fifa katika michezo ya Kombe la Dunia kwa kumtemea mate Roberto Carlos wa Brazil.

Mara tu baada ya Fifa kumwadhibu Chilavert alisema: “Huyu Roberto ni mpumbavu. Nilimtemea mate kwa vile alinionyesha mipira miwili aliyoificha ndani ya chupi. Mimi sio mke wake na nitakwenda kumchapa hata mbele ya mkewe au Rais wake.” Kwa miaka 14, kuanzia 1989 mpaka 2003, Chilavert alikuwa mlinda mlango namba moja wa Paraguay na kuichezea michezo 74 na kustaafu mwaka 2003.

Mara nyingi siku hizi huenda kuangalia mpira na licha ya umri mkubwa hugombana na kupigana na mashabiki.

IVAN ZAMORANO

Mchezaji mwengine aliyekuwa na vituko ni mshambuliaji mahiri wa zamani wa Chile, Ivan Luis Zamorano. Alikuwa mmoja wa wachezaji wazuri wa miaka ya 1990 na kuwamo katika kikosi cha Chile kilichocheza fainali za Kombe la Dunia za 1998. Alizichezea klabu maarufu za Sevilla na Real Madrid za Hispania na Internazionale Milan ya Italia. Mwaka 2004, alichaguliwa na Fifa mmoja wa wachezaji 100 bora waliokuwa hai ilipoanza karne ya 21.

Alipoichezea Real alikuwa akivaa jezi namba 9, lakini aliposajiliwa Ronaldo De Lima wa Brazil alitakiwaa kumuachia namba hiyo Ronaldo.

Hapo ndipo alipotoa kali na kutaka avae jezi yenye nambari 900 mgongoni, 9,000 kifuani na 90,000 kwenye kaptula. Alitaka namba 900 iwe katika maandishi ya Kiarabu na 90,000 maandishi ya Kigujerati (Kihindi).

Alisema ilikuwa bora kuhukumiwa kifo kuliko kumnyang’anya nambari 9.

Alisema mgongo wake uliipenda namba 9 kama alivyompenda mke wake na hakuwa tayari kupokea nambari nyingine. Baada ya mjadala mrefu alikubali kuvaa jezi namba 18, lakini alitumia namba 1 na 8 kuandika 1 na 8 huku alama ya kujumisha ikiwa katikati. Hii ilifanya jezi yake kuwa na maandishi yaliyosomeka 1+8 na hivyo kuwa na jumla ya 9. Alipoulizwa kama angepigwa marufuku kutumia namba ya 1+8 alisema angevaa jezi yenye namba 10-1 na kwa hivyo jawabu ingekuwa 9. Kama na hilo lingekataliwa angevaa jezi yenye maandishi ya “Nine” (9). Alisema alikuwa anafanya juhudi mke wake azae watoto tisa na akifa tarehe 10 au 21 ataomba mazishi yasubiri mpaka tarehe 9 ya mwezi unaofuata.

Zamorano alipewa na mashabiki wa kandanda wa Chile jina la utani laBam Bam (jina la michezo ya kuigiza wa zaidi ya nusu karne iliopita).

Zamorano) alienda Mexico mwaka 2001 na kuichezea America kwa misimu miwili na kustaafu kucheza soka la kulipwa akiwa na klabu ya Colo-Colo ya Chile mwishoni mwa mwaka 2003. Siku hiyo aliingia uwanjani tumbo wazi akiwa amechorwa nambari 9 na baadaye ndiyo akavaa jezi. Timu ya taifa ya Chile aliichezea mara 69 na kuifungia mabao 34.

EMMANUEL NEGRETE

Mchezaji mwengine ambaye vituko vyake vinavunja mbavu ni Emmanuel Negrete wa Mexico.

Siku moja katika mchezo wa ligi ya Mexico aliwala chenga walinzi na akibakia na golikipa alisimama, akainama na kuubusu mpira na baadaye aliuchota ukampita golikipa juu ya kichwa na kwenda wavuni.

Negrete aliutoa mpira wavuni na badala ya kwenda katikati ya uwanja ili mchezo uendelee alimpa golikipa na kumtaka aubusu na kumwambia hauna makosa na aliyefanya kosa ni yeye kwa kuusukuma wavuni. Negrete alipoulizwa na waandishi wa habari kwa nini alijiamini kupita kiasi alisema: “Ninapokuwa uwanjani huhisi mimi ni dereva wa gari na wachezaji wa upinzani ni abiria wangu na wanapaswa kwenda ninakotaka kwa vile nimeshika usukani.” Tofauti na wachezaji wengi mashuhuri wa miaka ya 1950, Negrete alitumia muda mwingi kuchezea klabu ndogo na alianza soka la kulipwa 1980 akiwa na miaka 30 alipojiunga na Universidad Nacional ya Mexico.

Kila alipotaka kusajiliwa kama mchezaji wa kulipwa alisema bado alikuwa mtoto mdogo na kuwaomba waliotaka kumsajili wasubiri apevuke kiumri. Alipojiunga na Unervsidad akiwa na umri mkubwa aliulizwa kwa nini alikawia kucheza soka la kulipwa jawabu lake ilikuwa kali kama mashuti yake. Alisema: “Hata nje ya uwanja wa kandanda wapo wanaofunga ndoa mapema na wengine wanakawia hadi wafikapo miaka 50 na zaidi. Uamuzi ni mapenzi ya mtu na siyo vizuri kumuingilia mtu katika mapenzi yake.

Ninaamini hata baadhi yenu baba zenu wamekawia kufunga ndoa.”

Alipoambiwa mchezo wa kandanda unahitaji nguvu za misuli ambazo huwa katika hali nzuri mtu anapokuwa kijana alisema: ”Kila kitu hakiwi mpaka ufike wakati wake. Hata katika uzazi wapo wanaozaliwa miezi saba, tisa au 10. Wengine hutaka kuendelea kubaki tumboni na ndipo mama hufanyiwa upasuaji”.

Negrete baadaye alikwenda Ureno na kujiunga na Sporting Lisbon na kumalizia na Atlante, Toros Neza na Acapulco. Alipostaafu kucheza soka la kiushindani alikuwa na miaka 40 na alisema labda akifikia miaka 50 atafikiria kurudi uwanjani kwani alikuwa anapumzika kwa muda.

Aliifungia Mexico mabao 57 katika mechi za mashindano na michezo ya kirafiki. Baada ya kustaafu Negrete alizifundisha timu za vijana nchini Mexico.