Kwa hili la Manji na Yanga, busara inahitaji zaidi

Muktasari:

Suala la Yusuph Manji ndani ya kikosi cha Yanga limechukua sura nyingine baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwaagiza Yanga kufanya uchaguzi kuziba nafasi zilizowazi ikiwemo ya Manji.

KWA wiki kadhaa sasa miongoni mwa mambo yanayogonga vichwa kwenye michezo ni suala la Yusuf Manji kama atarejea na kuendelea na wadhifa wake wa Mwenyekiti ama la.
Manji, ambaye anatajwa kama mtu aliyeiweka Yanga kwenye ramani ya soka barani Afrika, aliamua kuandika barua ya kujiengua katika nafasi hiyo baada ya kupatwa na misukosuko ya kibiashara.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kujindoa kwenye nafasi hiyo haukuwa umeungwa mkono na wanachama na viongozi wenzake hivyo, uamuzi wake huo haukuwa na baraka za wanachama waliomchagua kwenye Mkutano Mkuu.
Lakini, kwa sasa suala la Manji limechukua sura nyingine baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuwaagiza Yanga kufanya uchaguzi kuziba nafasi zilizowazi ikiwemo ya Manji. Nafasi zingine ambazo zinatakiwa kujazwa ni Makamu Mwenyekiti ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Clement Sanga, ambaye naye aliamua kuachia ngazi baada ya maji kuzidi unga. Pia, zipo za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao baadhi waliachia ngazi pia.
Agizo la BMT ambalo liliwataka Yanga kufanya uchaguzi huo chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, umeonakana kupokewa kwa hisia tofauti na kupitia viongozi wa matawi, kugomea mpango huo huku wakisisitiza kuwa Manji bado ni kiongozi halali wa Yanga.
Msimamo wa Yanga ulitolewa baada ya kumalizika kwa kikao cha wenyeviti wa matawi wa klabu hiyo, uliofanyika Makao Makuu ya klabu hiyo Jangwani, ambapo Mwenyekiti wa Matawi Bakili Makele alitoa msimamo huo.
Katika taarifa yake hiyo, Makele alisisitiza kuwa bado wanamtambua kuwa mwenyekiti wao na yupo ndani ya klabu hiyo akiendelea na majukumu yake kwa sasa.
Tamko hilo la Yanga kupitia Makele limeanza kuonekana kuwatibua TFF na kuamua kumuita mbele ya Kamati ya Maadili ya TTF kumhoji ni kwanini anapinga na uamuzi uliotolewa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za shirikisho hilo ambalo ndio lenye mpira wake.
"Mwenyekiti alipitishwa na wanachama katika mkutano mkuu na katiba inaruhusu kufanya hivyo, TFF nao baada ya kuona mwenyekiti yupo walimuondoa Clement Sanga kwa sababu wameona Manji bado yupo, sasa inakuwaje BMT waseme tuzibe nafasi hii," alikaririwa Makele.
Pia, alikaririwa akisisitiza kuwa baada ya kupata mapendekezo ya wanachama, wanapeleka uamuzi huo kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga pamoja na Bodi ya Wadhamini kwa hatua zaidi.
Kimsingi, Mwanaspoti linaamini kuwa TFF ambao ndio walezi na wasimamizi wa soka wanapaswa kukaa chini na viongozi wa Yanga na kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Tunasema hivyo, kwa sababu Manji ambaye ndio amekuwa kama mhusika mkuu amekuwa kimya huku yakitoka matamko kupitia viongozi wengine wanaosema kwa niaba yake.
Uamuzi wa Yanga kuendelea kukaidi ama kutaka kutunishiana msuli na TFF ama BMT hauwezi kuwa na faida kwa pande zote zaidi ya kuanzisha mgogoro ambao, mwisho wa siku unaweza kuzorotesha maendeleo ya soka.
Mabosi wa Yanga waliopo kwa sasa wanapaswa kutambua kuwa suala la uchaguzi bado linaweza kuwa na umuhimu kwa sababu, ndani yake kuna pande mbili zinazosigana wenyewe kwa wenyewe, moja ikitaka uchaguguzi na mwingine ukigomea.
Kuwepo kwa pande hizo ni kiashiria kwamba, mambo sio shwari sana na kuna jambo limejificha ndani yake na hapo ndipo busara inapaswa kufuata mkondo wake.
Yanga wanapaswa kuitisha mkutano mkuu na kuwahoji wanachama kama wanataka kuendelea na Manji ama kuchagua viongozi wengine na ikiwezekana mwenyewe awepo na kuweka msimamo tofauti na hali ilivyo sasa. Bado kuna wingu zito mbele.
Kwa upande wa TTF nako wanapaswa kulichukulia suala hilo kwa umakini zaidi badala ya kujikita kwenye kuwaita viongozi kuwahoji ili kupata fursa ya kuwaadhibu kwa kuwa, hapo itakuwa ni kuongeza tatizo badala ya kumaliza kwa njia sahihi wakiwa kama wasimamizi wa soka letu.
Tunasema hivyo kwa sababu, jana Alhamisi TTF imemuhoji Makele kupitia Kamati ya Maadili hivyo, kama itamkuta na hatia anaweza kuchukuliwa hatua ambazo kwa uongozi huu imekuwa na staili ya kuwafungia wadau wa soka kifungo cha maisha.
Hadi sasa, kamati hiyo ya maadili ya TFF chini ya Wakili Hamidu Mbwezeleni imeshatoa adhabu ya kifungo cha maisha ya kutojihusisha na soka kwa wadau wanne wa soka akiwemo Michael Wambura, Dastan Nkundi, Mbasha Matutu na Wakili Revocatus Kuuli huku pia likitoa adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja kwa aliyekuwa meneja wa Simba, Robert Richard.