Kwa Sarpong, wape salaam!

KIUNGO wa Prisons, Lambert Sabiyanka amesema licha ya kutoka na faida ya pointi moja dhidi ya Yanga, amefichua jinsi straika wa Wanajangwani Mghana, Michael Sarpong alivyowalaza mabeki wao na viatu.

Sabiyanka alitoa ushuhuda wa dakika 90 za Sarpong, kwamba aliwakimbiza mwanzo mwisho, akitumia akili za kulisakama goli lao, huku akilazimisha mashambulizi kwa nguvu bila kuogopa mabeki, kitu alichokiona ni chatofauti na washambuliaji wengine.

Alisema kwa uwezo aliouonyesha Sarpong wa kucheza kwa kujitolea kwa timu yake, anaamini anaweza akapindua meza kwa straika wa Simba, Meddie Kagere aliyechukua kiatu cha dhahabu mara mbili mfululizo.

Msimu wa 2018/19 Kagere alimaliza na mabao 23 na huu ulioisha nao alikuwa kinara wa mabao 22, jambo ambalo Sabiyanka anaona Sarpong anaweza akavunja rekodi hizo akiendelea kujituma.

“Sarpong ni mchezaji ambaye aliwapa kazi kubwa mabeki wetu ndani ya dakika 90, muda mwingi alikuwa analazimisha kwenda kwenye goli letu, kama angekabwa bila nidhamu basi wangepata faulo ambazo ingetugharimu,” alisema Sabiyanka na kuongeza:

“Siri ya kuambulia pointi moja, tulicheza kwa nidhamu zilizozidi asilimia 100, tulijua Yanga ina wachezaji wazoefu ambao walitaka kuonyesha kitu mbele ya mashabiki wao. Kocha alituambia tusiipuze dakika hata moja na kuwaachia watutawale,” alisema Sabiyanka.

Alisema kipindi cha pili ndicho kilikuwa kigumu kwao, akitoa sababu kwamba mastaa wa Yanga walikuwa wanasaka pointi tatu kwa hali na mali, huku na wao wakihitaji ushindi ama sare, hivyo walitimiza malengo yao.

GOLI LAKE

Alisema mazoezi waliyoyafanya siku mbili kabla ya mechi, alifunga mabao 10 ambayo yalitokana na kuzingatia maelekezo ya kocha wake Salum Mayanga, ambaye alikuwa anamtaka asifanye mbwembwe zaidi ya kuelekeza mipira golini.

“Baada ya mazoezi hayo, kocha alinifuata na kuniambia katika mechi ya Yanga hautatoka bure, lazima utafunga hivyo niliingia na ujasiri huo, hivyo sijabahatisha kufunga bao hilo, lililoipa heshima timu yetu kuanza ugenini kwa kishindo,” alisema.

Alisema alimsoma kipa wa Yanga, Farouk Shikalo alimuona akili yake inawaangalia mabeki wake kuokoa mpira, hivyo yeye akaamua akafanya uamuzi wa kupiga shuti la mbali lililozaa bao.

“Ilikuwa mechi ngumu, ambayo imetoa taswira ya msimu huu si wa kupata matokeo kirahisi, binafsi nitakwenda kuongeza juhudi ya mazoezi ili moto wangu usipoe,” alisema.

Tangu siku ya kwanza Sarpong alisema; “Siyo msemaji sana, ila mashabiki wao ndio wataona nafanya nini uwanjani, kikubwa wanipe ushirikiano wa kutosha ili kwa pamoja tufanye kitu kizuri kwa msimu huu.”