Kutoka Galacticoz mpaka N’Golo Kante, heshima imerudi

Muktasari:

Mwaka 2001, akamnunua Zinedine Zidane. Mwaka 2002 akamnunua Ronaldo Nazario Luis de Lima. Mwaka 2003. Akamnunua David Beckham. Akafunga hesabu zake za kununua Galacticoz. Tayari ndani ya nyumba alikuwa na Roberto Carlos na Raul ambao walikuwa mastaa.

JINSI maisha yalivyo na haraka. Julai 17, 2000, mtu anayeitwa Florentino Perez alikalia kiti cha ofisi yake ya Santiago Bernabeu kwa mara ya kwanza kama Rais. Akachukua peni yake ya dhahabu, akachukua kitabu cha Hundi akaanzisha utawala wa Galacticoz.

Hundi ya kwanza ilikwenda ofisi za Barcelona. Midomo wazi. Akamnunua Luis Figo. Sio kwamba Barcelona walitaka, hapana, Perez alikuwa ametengua tu kipengele cha mkataba wa mauzo ambacho kilionyesha kiasi cha pesa ambacho Figo angeruhusiwa kuondoka kama kuna timu ambayo ilimuhitaji.

Wakati Barcelona wanaweka kiwango cha pauni 37 milioni katika mkataba wa Figo walidhani kwamba hakuna klabu ambayo ingeweza kutoa. Kilikuwa kiasi kikubwa cha pesa. Perez alipeleka  hundi hiyo kwa Barcelona bila ya kupunguza senti moja.

Mwaka 2001 akamnunua Zinedine Zidane. Mwaka 2002 akamnunua Ronaldo Nazario Luis de Lima. Mwaka 2003. Akamnunua David Beckham. Akafunga hesabu zake za kununua Galacticoz. Tayari ndani ya nyumba alikuwa na Roberto Carlos na Raul ambao walikuwa mastaa.

Alipomaliza kununua Ferrari zake alisahau kuendelea kuwa na gari ngumu kama Fusso kwa ajili ya kuendea shambani. Eti akamuuza Claude Makelele kwenda Chelsea kwa kugoma kumlipa mshahara mkubwa aliotaka ambao ungeweza kumsogeza walau nusu ya anga za Galactico.

Ilikuwa dharau kwa viungo wakabaji. Kama vile haitoshi, aligoma kumnunua Patrick Vieira kutoka Arsenal. Kisa? Vieira alitaka mshahara mkubwa ingawa sio kama ule ambao walikuwa wanalipwa akina David Beckham.

Jahazi la Galacticos likaanza kuzama hapo. Nani amfanyie kazi nani? Unapowapanga akina Beckham, Figo, Ronaldo de Lima, Raul na Zidane kwa pamoja timu inakosa uwiano. Nani akabe? Nani awafanyie wenzake kazi ya punda?

Majuzi nilikuwa naangalia jinsi ambavyo wanahaha kumuongezea mkataba kiungo wao, N’Golo Kante. Wanataka kumlipa kiasi cha pauni 290,000 kwa wiki. Kwa sasa analipwa kiasi cha pauni 150,000. Kumbakisha Kante Stamford Bridge, Chelsea wanalazimika kupambana hasa?

Kwanini Chelsea wanapambana? Mpira wa kisasa. Jibu lake ni mpira wa kisasa. Walau dunia inaanza kuwaheshimu watu wanaofanya kazi ngumu ambao thamani zao haziwezi kulingana na Ferrari uwanjani. Eden Hazard atabakia kuwa Eden Hazard, na N’Golo Kante atabakia kuwa N’Golo Kante.

Wakati Hazard, kama ilivyo kwa wale galactico anabakia kuwa mchezaji alama ya timu, lakini kumbe kuna watu wanaofanya kazi ngumu maeneo mengine. Mara nyingi wachezaji wanaofanya kazi za Punda huwa hawaheshimiki. Kuna sababu mbili.

Kwanza kabisa hawatazamiki kistaa. Ni kama ilivyokuwa kwa Makelele. Ukimtazama kwa sura tu hana mvuto. Kama ilivyo kwa Gilberto Silva. Kama ilivyo kwa Kante sasa hivi. Haliwezi kupita tangazo la biashara halafu akatokea Kante. Hana sura ya mauzo.

Lakini pili ndani ya uwanja wanaangaliwa zaidi wachezaji wanaofunga. Kante hawezi kufunga hata mabao matano ndani ya msimu mmoja. Hata hivyo kazi anayoifanya  ni zaidi ya kufunga mabao 20 katika msimu.

Bahati nzuri Kante amepata bahati ambayo Makelele hakuipata. Mchezo wa soka unazidi kuwa wa Kisayansi zaidi na hatimaye wachezaji wanaokimbia zaidi uwanjani huku wakifanya kazi ngumu zisizoonekana kwa urahisi wameanza kupata thamani.

Mchezo wa soka umekuwa wa takwimu zaidi na sasa ni rahisi kutambua umuhimu wa mchezaji kama kante. Namba hazidanganyi na wachezaji wa aina yake wamekuwa na umuhimu mkubwa ambao unaelekea kulingana na hata wanaofunga.

Pale Arsenal ameingia Lucas Torreira. Amerekebisha matatizo yao ya muda mrefu katika eneo la kiungo. Kazi anayofanya ni ile ile ambayo Kante anaifanya Chelsea. Kufunga mabao halijawahi kuwa tatizo katika kikosi cha Arsenal, lakini ukabaji na ugumu eneo la katikati limekuwa tatizo la muda mrefu.

Kama Perez angeamua kukiunda kikosi cha galactico leo nadhani angemchukua N’Golo Kante kwa ajili ya kuwalinda mastaa wake. sidhani kama angerudia kosa lile lile alilolifanya katika zama za Claude Makelele. Mabadiliko ya mchezo wa soka ndani ya uwanja yanalazimika zaidi.

Kwa sasa pia hata makipa wananunuliwa kwa pesa ndefu na wanalipwa pesa ndefu. David De Gea anakaribia kulipwa kiasi cha pauni 300,000 kwa wiki pale Old Trafford. Hapana shaka atakuwa analipwa pesa ndefu kuliko washambuliaji wake kikosini. Zamani usingemlipa kipa pesa nyingi kuliko mshambuliaji.

Wakati fulani bosi wa Barcelona, Joan Laporta alitoa maneno ya dharau kwa Victor Valdes kwamba hakustahili kupata mshahara mkubwa Nou Camp kwa sababu kazi yake ilikuwa rahisi na muda mwingi Barcelona walikuwa wanashambulia kuliko kujihami.

Hili la Kante linarudisha heshima kwa wachezaji wa nafasi yake. Kuanzia nyakati za Galacticos mpaka sasa ni wazi kwamba Kante na wenzake wanaocheza kwa shoka katika eneo hilo wamejaribu kupindua ubao wa dharau uliokuwa unawakabili.