Kusajili mastaa wa Kingereza lazima uvunje benki unaambiwa

Muktasari:

Hii hapa ndio tano bora ya orodha ya wanasoka wa Kingereza waliosajiliwa kwa mkwanja mrefu katika historia ya Ligi Kuu England.

LONDON,ENGLAND.WACHEZAJI wa Kiingereza huwa hawapatikani kirahisirahisi, lazima umwage pesa. Ni hivyo, ndiyo maana Leicester City inahitaji ilipwe Pauni 80 milioni kwenye mauzo ya beki wake wa kati, Mwingereza Harry Maguire, anayesakwa na Manchester City na Manchester United.

Ripoti zimedai Man City ipo tayari kulipa kiwango hicho cha pesa ili kupata huduma ya beki huyo wa kati, ambaye imepanga kwenda kumlipa mshahara wa Pauni 280,000 kwa wiki baada ya kocha wake, Pep Guardiola kuhitaji mrithi wa Vincent Kompany.

Ada hiyo itamfanya Maguire kuwa beki ghali zaidi duniani na kuongezeka kwa wanasoka wa Kingereza walionaswa kwa pesa nyingi katika miaka ya karibuni.

Hii hapa ndio tano bora ya orodha ya wanasoka wa Kingereza waliosajiliwa kwa mkwanja mrefu katika historia ya Ligi Kuu England.

5. Luke Shaw - Pauni 30 milioni

Mwaka 2014, Manchester United ilifungua pochi na kutoa Pauni 30 milioni kuilipa Southampton kwa ajili ya kupata huduma ya beki wa kushoto, Luke Shaw. Kwa wakati huo, jambo hilo lilimfanya Shaw kuwa beki wa Kingereza aliyenaswa kwa pesa nyingi tangu mwaka 2002, wakati Man United ilipolipa kiasi kama hicho cha pesa kunasa huduma ya beki wa kati, Mwingereza Rio Ferdinand kutoka Leeds United. Ada yake Shaw inamfanya kuwamo kwenye orodha ya wachezaji wa Kingereza walionaswa kwa pesa nyingi.

4. Andy Carroll - Pauni 35 milioni

Kwenye dirisha la Januari 2011, Liverpool ilipiga hodi huko Newcastle United na kwenda kunasa huduma ya mshambuliaji Andy Carroll, aliyekuwa moto kwa kipindi hicho.

Kwa wakati huo, Liverpool ilikuwa na pesa baada ya kumpiga bei Fernando Torres kwenda Chelsea kwa ada ya Pauni 50 milioni.

Kutokana na hilo, Kocha Kenny Dalglish alitoa ruhusa ya kwenda kusajili Carroll kwa Pauni 35 milioni, ambazo zinamfanya awe mmoja kati ya wanasoka ghali kabisa wa Kingereza hadi sasa. Mabao 11 katika mechi 19 alizocheza Newcastle ilitosha kumfanya Carroll atue Anfield.

3. John Stones - Pauni 47.5 milioni

Mwaka 2016, Manchester City iliandika rekodi kwa kusajili beki kwa pesa nyingi zaidi wakati ilipolipa Pauni 47.5 milioni kunasa saini ya John Stones kutoka Everton.

Msimu wake wa kwanza Stones huko Etihad ulikuwa wa mapito makubwa ambapo alisababisha makosa matatu yaliyozaa mabao kwa wapinzani, ambapo Man City ilimaliza nafasi ya tatu kwenye ligi bila ya kubeba taji lolote.

Baada ya hapo Stones alijiimarisha zaidi kwenye kikosi akicheza sambamba na Aymeric Laporte na kudhihirisha kwanini Pep Guardiola alitoa pesa yake nyingi kumsajili.

2. Raheem Sterling -Pauni 49 milioni

Manchester City tena iliingia kwenye rekodi ya kusajili mastaa wa Kingereza kwa pesa nyingi wakati ilipokwenda Liverpool na kumng’oa Raheem Sterling kwa ada ya Pauni 49 milioni.

Uhamisho huo uliofanyika mwaka 2015. Sterling kwa siku za karibuni amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha Man City hasa baada ya ujio wa Kocha Pep Guardiola kwenye kikosi hicho cha Etihad.

Kiwango cha Sterling kimethibitisha pesa halisi iliyolipwa kunaswa huduma yake kutokana na ukweli kwamba ameisaidia timu hiyo kunasa mataji ya Ligi Kuu England kwa misimu miwili mfululizo.

1. Kyle Walker - Pauni 53 milioni

Pengine Manchester City ndiyo inayowathaminisha zaidi wanasoka wa Kingereza kutokana na ukweli kwamba wanasoka ghali watatu wa juu wa Kingereza, wote wamesajiliwa na wababe hao wa Etihad.

Wakati sasa Man City ikiwa tayari kutoa pesa ndefu zaidi kuinasa huduma ya beki wa kati Harry Maguire, mwaka 2017 ilitoa mkwanja wa Pauni 53 milioni kumnyakua beki wa pembeni, Kyle Walker kutoka Tottenham Hotspur.

Hadi sasa ikiwa hakuna beki mwingine Mwingereza aliyenaswa kwa pesa nyingi, Walker anashikilia rekodi ya kuwa beki ghali zaidi wa Kingereza huko kwenye Ligi Kuu England.