Kurasini Heat bingwa mpya RBA

Kurasini Heat imepindua meza na kutwaa ubingwa wa Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) msimu huu.

 

Timu hiyo imeweka rekodi iliyoisotea kwa miaka 11, jana usiku baada ya kushinda mechi ya tatu mfululizo na kutawazwa kuwa bingwa mpya msimu huu.

 

Kurasini Heat imeichapa JKT pointi 64-61 katika mechi ya nne ya fainali (game 4), katika mchezo uliokuwa na upinzani wa hali ya juu kwenye uwanja wa Bandari Kurasini.

 

"Ilikuwa ni lazima tushinde, kwa miaka 11 mfululizo hatukuwahi kufuzu fainali, mwaka huu tulipofuzu, tuliweka malengo," anasema kocha Shendu Mwagalla wa Kurasini Heat.

 

Alisema walipofungwa mechi ya kwanza ya fainali (64-57) walifanya 'review' (marejeo) na kubaini makosa waliyofanya sambamba na ubora wa JKT na kuufanyia kazi.

 

"Tulitumia mbinu ya kuwazuia wachezaji wao wasifunge, tukafanikiwa kwenye mechi ya pili na kushinda, vivyo hivyo mechi ya tatu (walishinda pointi 78-77) na ya jana usiku," alisema.

 

Kurasini Heat imetwaa ubingwa kwa matokeo ya ushindi wa mechi 3-1 na kuandika rekodi ya ubingwa kwa mara ya kwanza tangu ilipoanzishwa kwanza 2009.

 

"Hatukuwahi kuingia fainali tangu mwaka huo, tulipofuzu hatua hiyo mwaka huu, ilikuwa ni chachu ya kuhakikisha hatupotezi nafasi hiyo," amesema.

 

S.JKT imemaliza ya pili na Oilers ikihitimisha tatu bora msimu huu baada ya kuichapa ABC kwa pointi 55-52 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu hivi karibuni ambao ulichezwa katika mzunguko mmoja (game one).