Kumbe babu Wenger kamtia hasira Modric

Thursday December 6 2018

 

MADRID, HISPANIA.MWANASOKA Bora wa Dunia, Luka Modric amefichua Kocha Arsene Wenger ndiye aliyemfanya kuwa na hasira ya kupiga soka la kiwango kikubwa kufikia mafanikio aliyopata kwa sasa.

Staa huyo wa kimataifa wa Croatia, anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid alisema huko nyuma alikataliwa na Kocha Wenger wakati Arsenal ilipotaka kumsajili kwenye kikosi chake na jambo hilo lilimfanya Modric kuwa na hasira ya kutaka kucheza kwa kiwango cha juu ili amwonyeshe Mfaransa huyo makosa yake aliyofanya kwa kumkataa.

Modric alikwenda kuichezea Tottenham Hotspur, mahasimu wa Arsenal kabla ya kwenda kujiunga na Real Madrid ambako ubora wake umemfanya ashinde Tuzo ya Ballon d’Or Jumatatu iliyopita, huku akibeba tuzo nyingine kadhaa za ubora ndani ya mwaka huu kutokana na soka lake matata alilocheza akiwa na timu ya taifa ambayo aliifikisha fainali ya Kombe la Dunia 2018 huko Russia.

Modric alisema huko nyuma angeweza kujiunga na Arsenal, lakini Kocha Wenger alimkataa na hivyo alilichukua jambo hilo kama changamoto chanya katika kumfanya kufikia malengo yake ya kucheza soka la juu.

“Nililichukulia lile suala la kukataliwa na Wenger kama hamasa katika kupambana na mambo kama hayo mbele ya safari. Hilo ndilo lililokuwa akili mwangu kwa wakati ule,” alisema Modric.

Advertisement