Kumbe Morrison aliiga hapa

STAILI ya ushangiliaji ya winga wa Simba, Benard Morrison kwa hapa Tanzania kumbe hakuibuni yeye buana, Thomas Kipese amethibitisha kwamba ndiye aliyeiasisi.

Morrison ameonekana kivutio kwa mashabiki nchini kwa staili aliyoianzia Yanga alipokuwa akishangilia kwa kunyanyua mguu mmoja juu, huku akitambaa chini, jambo lililomuibua mwanzilishi wa hiyo staili hapa nchini.

Kivutio zaidi kilikuwa Machi 8, mwaka huu, Morrison alipoitungua Simba katika mchezo wa watani wa jadi wakati huo akiichezea Yanga, hivyo kukimbia hadi karibu na mashabiki wa Simba na kutambaa huku akishangilia kwa staili hiyo.

Straika wa zamani wa Simba na Yanga, Thomas Kipese ‘Uncle Tom’ alisema kwa hapa Tanzania yeye ndiye mwanzilishi wa staili hiyo, ambapo kwa mara ya kwanza alishangilia Simba ilivyocheza na CDA ya Dodoma mwaka 1993.

“Hiyo staili niliona kwa mchezaji mmoja wa timu ya taifa ya Nigeria, baada ya kufunga akawa ananyanyua mguu mmoja juu, huku akiwa anatambaa, niliipenda, hivyo nikawa naifanya wakati nipo na Simba,” alisema Kipese

“Siku nilivyoshangilia hivyo baada ya kuwafunga CDA, ilikuwa kivutio kwa wengi, kama vijana wa sasa wanavyovutiwa na Morrison, ndio maana nasema hakuianza yeye (Morrison) ilikuwepo tangu zamani.”

Kipese alisema kitu kinachomfurahisha zaidi ni aina ya ufundi na udambwidambwi alionao Morrison katika mguu wake, kwamba laiti kama kungekuwepo na kumbukumbu za video walivyokuwa wanacheza zamani, basi mengi yasingekuwa mapya kwa sasa.

“Tulifanya mengi zamani kama wao, lakini kwa sababu hakuna ushahidi wa hayo kwa njia ya video ndio maana yanaonekana mapya, ila wahenga wenzetu wanaelewa ninayoyasema kuwa ni kweli na pengine tulicheza zaidi yao,” alisema.