Kumbe Jose Mourinho alitibua Pulisic kutua Manchester United

Muktasari:

Robin Walker, ambaye amemfundisha Pulisic tangu akiwa mdogo kwenye klabu ya Brackley Town, alisema kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Chelsea kwa kuwa amekulia na kuishi jijini London.

Manchester,England.GARI la Chelsea ya Frank Lampard bado halijachanganya japo limeanza kuonyesha dalili njema hapo baadaye. Hilo linatokana na uwepo wa damu changa ndani ya kikosi cha wababe hao wa Darajani akiwemo Christian Pulisic.

Pulisic alinaswa na Chelsea msimu uliopita kwa dau la Pauni 58 milioni, kisha akaachwa kwenye klabu yake ya zamani ya Borrusia Dortmund na msimu huu ameanza rasmi kuitumikia klabu yake mpya.

Awali, Chelsea ilikuwa ikipambana na Manchester United katika kuwania saini ya kinda huyo wa Dortmund, na iliaminika kabisa kwamba angetua zake Old Trafford, lakini ghafla tu mambo yakabadilika.

Hata hivyo, siri ya Pulisic kuigomea Man United na kukubali kusaini Chelsea, sababu kubwa ni Jose Mourinho.

Mreno huyo aliliweka kwenye orodha ya juu jina la Pulisic na mabosi wake walikuwa tayari kuweka ofa nono mezani, lakini kinda huyo akachomoa.

Imebanika kuwa uamuzi wa Pulisic kugomea kutua Old Trafford ulitokana na baba yake kutovutiwa na sera ya Mourinho ya kuwanyima nafasi makinda kuonyesha vipaji vyao.

“Baba yake hakuwa upande wake kwenye dili la kutaka kwenda Man United. Sera za Mourinho kutopenda kuwatumia na kuwaendeleza vijana wenye vipaji zilimtisha,” amefichua mmoja wa makocha wa zamani wa kinda huyo mwenye miaka 20.

Robin Walker, ambaye amemfundisha Pulisic tangu akiwa mdogo kwenye klabu ya Brackley Town, alisema kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Chelsea kwa kuwa amekulia na kuishi jijini London.

“Hakutaka kuchezea Man United kwa sababu wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Jose Mourinho. Baba yake Pulisic sio mfuasi wa Mourinho, kwa sababu ya kutopenda kuwapa nafasi vijana. Sababu ilikuwa hiyo tu vinginevyo angekuwa yuko Old Trafford kwa sasa,” alisema Walker.

Mbali na Pulisic, Man United pia iliwakosa wachezaji wengi mastaa iliokuwa ikiwasaka kutokana na kutovutiwa na sera za Mourinho hasa za kuwakosoa hadharani.

Desemba mwaka jana, mabosi wa Man United walifikia uamuzi wa kumfuta kazi Mourinho na nafasi yake kuchukuliwa na Ole Gunnar Solskjaer, ambaye amekuwa akiwaamini vijana uwanjani.

Katika utawala wa Mourinho, makinda wenye vipaji kama Andreas Pereira, Scott McTominay, Tahith Chong, Gomes na Mason Greenwood hawakuwa wakipewa nafasi kuonyesha uwezo wao.

Lakini, kwa sasa Ole amekuwa akiwatumia vijana hao hata kwenye mechi kubwa wakicheza sambamba na nyota wapya Daniel James na Aaron Wan-Bissaka.

Kwa sasa, Pulisic ndiye anatajwa kama mrithi wa Mbelegiji Eden Hazard aliyetua Real Madrid huku Chelsea ikiendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa kufanya usajili mpya.

Nyota huyo ameanza kwenye mechi zote mbili za ufunguzi dhidi ya Manchester United pale Old Trafford ambako Chelsea ilichapwa bao 4-0 na juzi dhidi ya Leicetser City, uwanjani Stamford Bridge, iliyomalizika kwa sare ya 1-1.