Kumbe Alliance tatizo ni hili

BAADA ya timu ya Alliance kupoteza mfululizo michezo yote miwili kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu, kocha wa timu hiyo ametaja sababu za kukosa ushindi.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkuu wa timu hiyo, Dady Gilbert ameeleza kuwa tatizo kubwa linalowafanya kukosa ushindi ni wachezaji kutokuwa na uzoefu wa mashindano makubwa.

“Kwa bahati mbaya zaidi kwenye kikosi chetu msimu huu asilimia kubwa ya wachezaji hawajakuzwa na timu yetu (Alliance), wengi tumewachukua mtaani, kwa hiyo wanakuwa hawana uzoefu na mashindano makubwa kama haya,” alisema.

“Ukitazama mechi tulizofungwa utaona mabao mengi yanapatikana kwenye dakika 30 za mwanzo, ambapo wachezaji wanakuwa bado wana presha ya mchezo kwa kuwa ni wapya kwenye mashindano haya, ila baada ya hapo wanacheza vizuri japo wanakosa kufunga, nadhani hilo ndilo tatizo.”

Licha ya hayo. kocha Dady amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwaomba waendelee kuisapoti Alliance kwani huu ni mwanzo wa ligi na mabadiliko yanakuja.

“Kwa matokeo haya lazima wajisikie vibaya, lakini niwatoe shaka kuwa tumepoteza michezo miwili ya mwanzo na bado tuna safari ndefu, hivyo mabadiliko lazima yafanyike ili tupate matokeo chanya, wasichoke kuipa nguvu timu yao kwani naamini siku za neema kwa Alliance zinakuja,” alisema.

Mpaka sasa Alliance inashika nafasi ya mwisho (10) kwenye kundi B ikiwa imepoteza michezo miwili kwa kupigwa bao tatu bila kila mchezo dhidi ya timu za Fountain Gate FC na Transit Camp FC. Mchezo unaofuata a Oktoba 25 ni dhidi ya Geita Gold FC.