Kumbe ‘Hawa wa Diamond’ tatizo ni moyo siyo ini

Muktasari:

Msanii Hawa Said amegundulika kuwa ugonjwa unaomsumbua siyo ini bali ni moyo na sasa anatarajiwa kufanyiwa upasuaji kubwa ya moyo nchini India huku akiwaomba Watanzania waendelee kumuombea.

Dar es Salaam. Mwanamuziki Hawa Said maarufu kwa jina la Hawa wa Diamond amegundulika kuwa na maradhi ya moyo si ugonjwa wa Ini uliosemwa awali.

Hawa aliyeondoka nchini kwenda India Oktoba 13, mwaka huu, amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kujaa tumbo na miguu, katika matibabu aliyokuwa anapata katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ilisema tatizo hilo lilitokana na ugonjwa wa Ini.

Leo Oktoba 22 na Meneja wa Diamond Babu Tale kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Instagram akiwa ameweka picha ya Hawa alisema uchunguzi uliofanya na madaktari wa India umegundua ni tatizo la moyo si ini.

Babu Tale alielezea “Asante Mungu tumefika salama India na tumefanya vipimo vyote upya salama na jibu lililotoka kwa wataalamu kwa asilimia 95% awajaona tatizo linalohusiana na ini kwa mgonjwa ila ni moyo ndio uliokua unapelekea mgonjwa kujaa maji mwilini.

“Hivyo basi kutaitajika kufanyika upasuaji mkubwa ambao utakua na uangalizi mkubwa wa wataamu na wametuakikishia baada ya hapo mgonjwa atapata nafuu na inawezekana hizo asilimia tano zilizobaki itakua poa na tatizo la ini alitokuwepo kikubwa tunaomba mtuombee dua na msiache kumuombea pia Diamondplatnumz apate nguvu ya kuendelea kumsaidia kwa maana kutoa ni moyo.

“Kikubwa sana naomba tumuombee Hawa kwa kuwa anaingia kwenye upasuaji mkubwa na hii ni hatua ya yeye kuwaa salama. Mungu tusimamie,”ameandika Babu Tale.