Kumbe! De Bruyne kanyanyaswa kinoma

Muktasari:

  • De Bruyne ni mmoja kati ya nyota makini duniani, katika siku za karibuni alikuwa akisumbuliwa na maumivu lakini baada ya kurudi uwanjani, alirudi kwa kasi kubwa. Alijiunga katika kambi ya Etihad akitokea Wolfsburg kwa ada ya Pauni 54 milioni mwaka 2015.

LONDON,England.KEVIN DE BRUYNE ni jina kubwa katika soka kwa sasa. Hata hivyo, nyota huyo wa Manchester City ni miongoni wa wanasoka waliopitia changamoto kabla ya kufikia hatua kubwa katika soka. Yeye anasema alichagizwa kufika mbali kutokana na ‘hasira’.

Anasema kuna wakati familia iliyokuwa ikimlea ilimkataa bila sababu ya msingi ndio maana akashikwa na hasira ya maendeleo.

De Bruyne ni mmoja kati ya nyota makini duniani, katika siku za karibuni alikuwa akisumbuliwa na maumivu lakini baada ya kurudi uwanjani, alirudi kwa kasi kubwa. Alijiunga katika kambi ya Etihad akitokea Wolfsburg kwa ada ya Pauni 54 milioni mwaka 2015.

Asimulia yalomsibu

Mchezaji huyo kaibuka na kusema wazi alinyanyaswa akiwa na umri wa miaka 15 pekee huko Genk.

Klabu hiyo ya Ubelgiji ilimchukua na kumweka katika familia ya Foster kwa miezi 12 ili apate maisha bora na kujifunza vitu tofauti wakati akisubiri amalizie shule. Akiwa huko aliendelea na kufanya mazoezi katika akademi ya klabu hiyo. “Mwaka mmoja ulipita vizuri na nilikuwa nafanya vizuri shuleni na klabuni, hakukuwa na shida ya namna yoyote.

“Mwishoni mwa mwaka nilijipanga kwa ajili ya kurudi katika familia yangu halisi. Nilikusanya mabegi na kuanza kuondoka.

“Watu wa familia hiyo waliniaga vizuri na kuniambia: ‘Uwe na likizo njema. Tutakuona baada ya mapumziko, uwe na muda mzuri. Nilirudi nyumbani nikiwa na furaha ya kutaka kuonana na mama.Lakini baada ya kurudi katika nyumba ya familia yangu halisi nilimkuta mama kajiinamia huku analia.”

“Nilifikiri kuna mtu amekufa au kitu kibaya kimetokea, mama yangu aliniambia maneno ambayo sitokaa niyasahau daima. ‘Hawataki urudi kwao,’ alisema mama. “Nilimuuliza kwa nini?

“Akasema: ‘Wanasema kwa sababu ya hulka yako, wanadai eti upo kimya sana na hawawezi kukuzoea, wewe ni mgumu sana, huzoeleki. Hawawezi kuishi na mtu wa aina hiyo. “Nilishangaa sana, hilo lilikuwa ni jambo kubwa sana katika maisha yangu ya soka. Sikuwa nyota kwa wakati huo.

Aamua kujituma

Anasema baada ya tukio hilo alijiambia moyoni atawaonyesha watu hao hawakuwa sahihi. “Ninakumbuka, mama yangu alikuwa analia sana, niliumia sana. Nilitoka nje ya uzio ambako mara kwa mara nilikuwa nacheza na wenzangu.

“Neno pekee lilikokuwa likinirudia kichwani lilikuwa “Hawakutaki kutokana na hulka yako ya ukimya.” “Nilichukua mpira na kuanza kuupiga katika uzio kwa saa kadhaa. Nilipiga kelele nikiwa nje “kila kitu kitakuwa sawa.” Katika kipindi cha mwezi mmoja nitakuwa katika kikosi cha kwanza, sijali nitakumbana na nini, ninachojua sitarudi nyumbani nikiwa nimefeli. Nilifukuzwa katika nyumba ya awali lakini soka langu liliendelea, baada ya mwezi mmoja nilifanya juhudi na kutua kikosi cha kwanza.

Mambo yalivyonyooka

“Nakumbuka wakati mambo yalipobadilika, ilikuwa ni Ijumaa jioni, tulikuwa tukicheza ligi ya chini. Nilianzia benchi, baada ya kutua katika kikosi kwenye kipindi cha pili, nilikuwa kama kichaa, nilifunga mabao matano. “Baada ya hapo kila mtu katika klabu alifahamu mimi ni nani, niliitwa kikosi cha kwanza na baada ya miezi miwili nilipangwa kikosi cha kwanza.

“Siku moja mama wa familia ya Foster alikuja katika klabu na kuniambia nisijali sana, anadhani ujumbe haukufika vizuri, hawakumaanisha kile nilichokuwa nimesikia kutoka kwa mama yangu.

“Labda ningeona ni kawaida, lakini kwa wakati huo haikuwa kawaida. Nilichukia.

“Nilimwambia, mlinitupa majalalani, sasa mnaona ninafanya vizuri, mnataka nirudi. Haiwezekani.”