Kukosa usimamizi makini kunakatisha ndoto za mafanikio

Tuesday April 9 2019

 

KABLA ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, TP Mazembe ilishakuwa na Mtanzania aliyeitwa Ngawina Ramadhan Ngawina.

Hapa nchini Ngawina alichezea Kariakoo ya Lindi na baadaye Kahama United.

Mwaka 2003, alienda kucheza soka Rwanda katika klabu ya Mukura Victory, akipelekwa na Athumani Bilal, Bilo Bilongo, ambaye aliwachukua vijana 6 wa Kitanzania, akiwemo Jemedari Said.

Bilali alikuwa mzoefu nchini huko kwani tayari alishacheza miaka kadhaa nyuma yake kiasi cha kupewa uraia na kuitumikia timu ya taifa.

Walipofika huko, wengine maisha ya ugenini yakawashinda na kurudi nyumbani, lakini Ngawina akaendelea kupambana.

Mwaka huo, Rwanda ilifuzu kwa AFCON ya 2004 Tunisia, na katika kujiandaa, waliifupisha ligi yao ili iishe mapema kumsaidia kocha wa timu ya taifa kupata muda wa kujiandaa na wachezaji wake.

Ni katika ligi hiyo, ndipo Ngawina akakutana na mchezaji fulani wa DRC aliyemshauri waende Kongo. Alimwambia kwamba watapata klabu ndogo ambayo haitowalipa vizuri, lakini kwa viwango vyao, watapata klabu kubwa itakayowalipa vizuri zaidi.

Ngawina akaondoka na yule mchezaji hadi Kongo na kujiunga na klabu ya Bukavu. Na kweli, kupitia Bukavu Ngawina na mwenzake wakaonekana na klabu kubwa za DRC ambapo Lupopo, AS Vita na TP Mazembe zikaanza kupigana vikumbo.

Yule mchezaji aliyekuwa na Ngawina, aliitwa kwenye kikosi cha awali cha DRC kilichokuwa kikijiandaa na AFCON 2004.

Akiwa kambini Afrika Kusini, akakutana na Rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi Chapwe, ambaye alikubaliana naye kumlipa dola 6,500 kwa ajili ya Ngawina.

Wakati huo, Moise Katumbi Chapwe alikuwa katika mkakati wa kuisuka TP Mazembe irejee kwenye ubora wake.

Akamtuma afisa mmoja wa TP Mazembe kutoka Lubumbashi kwenda Goma kuwasubiri Ngawina na mwenzake kukamilisha dili.

Yule afisa akaja na zile fedha. Lakini yule wakala ambaye ni mchezaji mwenzake na Ngawina, akataka mgao wake na yule afisa naye akataka mgao wake. Ngawina akaishia kupata dola 2,000.

Ngawina na mwenzake walisajiliwa pamoja na Jean Kasusula huku Dieumerci Mbokani akifeli majaribio na kuachwa.

Kocha wa sasa wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe, ndiyo alikuwa nahodha. Pia alikuwepo Robert Kidiaba, pamoja na wengine wengi.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Ngawina kujiunga na TP Mazembe. Yule afisa aliyetumwa kuwasubiri Goma, hakumkubali Ngawina alipomuona kwa mara ya kwanza.

Pale Goma, Ngawina hakutaka kukaa bila angalau kufanya mazoezi. Akatafuta uwanja na kupasha na wenyeji.

Katika mazoezi hayo, alikuwepo kocha mmoja rafiki yake na Raoul Shungu, ambaye alifahamiana na yule afisa wa Mazembe.

Yule kocha alipomuona Ngawina pale mazoezini, akamuita yule afisa kumshuhudia mchezaji anayemdharau.

Yule afisa baada ya kumuona, pale pale akabadili mawazo na kuanza kumuamini.

Dili la Mzembe likakamilika na maisha mapya yakaanza pale Lubumbashi. Katumbi alikuwa na tabia ya kutoa dola 500 kwa kila mchezaji kila mwisho wa wiki. Bosi huyo akawa anachukua mgao wa Ngawina na kuupiga panga. Badala ya dola 500, anampelekea dola 100 na kusema, ‘hizi ni hela zako kutoka kwa bosi’. Hakumwambia kama ni mgao wa kawaida.

Mazembe walimsajili Ngawina wakijua ni Mkongo kutoka Bukavu, hawakujua kama ni Mtanzania. Lakini Ngawina alimwambia kigogo huyo kwamba yeye ni Mtanzania ila yule afisa hakutaka kuwaambia ukweli Mazembe.

Mwisho wa msimu, kila mchezaji alikuwa akipewa nauli ya kurudi nyumbani kwao.

Kwa kuwa Mazembe walijua Ngawina kwao ni Bukavu, wakampa dola 700 ambayo ndo ilikuwa nauli halisi.

Hata hivyo akalalamika kwamba kwao ni Dar es Salaam, Tanzania hivyo anatakiwa aongezewe hela. Mkubwa huyo akaanza kumtisha kwamba asiseme hivyo kwani klabu ikijua inaweza kumuacha.

Wachezaji wote wakaondoka, Ngawina akabaki kwenye hosteli za klabu. Yule afisa akamshauri achukue ile dola 700 halafu yeye atamuongezea zilizobaki.

Ngawina akakataa na kurudi nyumbani kwa nauli yake, akapanda Basi la Taqwa hadi Dar es Salaam. Alipofika nyumbani, akagoma kurudi Kongo.

Klabu ikamsubiri na kuamua kumpigia simu kujua kwanini harudi. Akasema atumiwe nauli. Lakini afisa huyo alianza kuhofia mawasiliano ya klabu na Ngawina, kwamba yatafichua machafu yake mengi.

Akaanza kumfanyia figisu klabuni. Akasema kwamba asitumiwe nauli kwa sababu hatorudi tena. Kwamba alishaanza mawasiliano na AS Vita, lakini pia anataka kwenda uarabuni.

Klabu ikasita kumtumia nauli, ikamwambia atumie nauli yake na atalipwa akirudi. Ngawina akagoma...na ndo ukawa mwisho wake.

Simulizi hii inaweza kukuonesha ni namna gani kukosa usimamizi sahihi kwa wachezaji kunavyowaathiri.

Endapo Ngawina angekuwa na usimamizi sahihi, TP Mazembe wangemheshimu kuanzia kwenye uraia wake, maana kusingekuwa na cha kuficha.

Lakini pia asingepoteza haki zake kwa kudhulumiwa na mtu aliyejipenyeza kati ilhali hakumsaidia lolote hadi kuifika alipofika. Pichani, Ngawina Ngawina akiwa na Robert Kidiaba na Jean Kasusula, walipokuja na TP Mazembe mwaka 2016 kucheza dhidi ya Yanga kwenye Kombe la Shirikisho.

Advertisement