Koulibaly ngoma bado ngumu Man United

Muktasari:

Ofa hiyo kubwa inayoipita kwa mbali ada ya Pauni 75 milioni iliyolipwa na Liverpool kwa ajili ya kumsajili Virgil van Dijk, inaonyesha United wamedhamiria kumaliza unyonge wao kwa mabingwa Manchester City.

OFA nzito ya Pauni 95 milioni kutoka Manchester United kwa ajili ya kutaka kumsajili beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly, imekataliwa.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Senegal anatajwa kama mmoja wa mabeki wa kati bora zaidi duniani kwa sasa na United wamedhamiria kuimarisha safu yao ya ulinzi inayovuja kama chujio.

Mwandishi wa gazeti la Gazzetta Dello Sport, Nicolo Schira, ameripoti ofa hiyo ya United ambayo ingevunja rekodi ya uhamisho kwa walinzi, imekataliwa na miamba hao wa Italia.

Ofa hiyo kubwa inayoipita kwa mbali ada ya Pauni 75 milioni iliyolipwa na Liverpool kwa ajili ya kumsajili Virgil van Dijk, inaonyesha United wamedhamiria kumaliza unyonge wao kwa mabingwa Manchester City.

Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, anajua chifu wa United, Ed Woodward, yuko katika presha ya kusajili ili kumsapoti Kocha Ole Gunnar Solskjaer na hayuko tayari kupokea ofa yoyote chini ya Pauni 130 milioni.