Kotei aitega Simba kimtindo

Muktasari:

Wachezaji Juuko Murshid (Uganda), Nicholaus Gyan (Ghana), Kotei na Niyonzima wako mguu ndani - nje kuhusu hatima zao za usajili kutokana mgawanyiko wa pande mbili za uongozi na benchi la ufundi.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikitarajia kuwapa mkono wa kwaheri wachezaji saba wa kigeni, kiungo Mghana James Kotei na Haruna Niyonzima raia wa Rwanda, wamewagawa vigogo wa klabu hiyo kongwe nchini.

Mabeki raia wa Ivory Coast, Zana Coulibaly, Asante Kwasi (Ghana) na Mganda Emmanuel Okwi hawatakuwemo katika usajili wa msimu ujao wa klabu hiyo.

Wachezaji Juuko Murshid (Uganda), Nicholaus Gyan (Ghana), Kotei na Niyonzima wako mguu ndani - nje kuhusu hatima zao za usajili kutokana mgawanyiko wa pande mbili za uongozi na benchi la ufundi.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema Kotei na Niyonzima wameibua mjadala mzito baada ya Kocha Patrick Aussems kupendekeza katika ripoti yake wakatwe.

Chanzo hicho kilisema pamoja na mapendekezo ya Aussems, vigogo wa klabu hiyo wamepinga uamuzi huo kwa madai kuwa Kotei na Niyonzima ni wachezaji wenye sifa ya kucheza Simba msimu ujao.

“Simba inatarajia kuacha wachezaji saba wa kigeni, lakini kuna mjadala unaendelea kuhusu ripoti ya mwalimu inayotaka Niyonzima na Kotei waachwe. Kocha anadai Niyonzima alimsumbua sana hivyo hawezi kuwa naye msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilidai nyota watatu pekee wana uhakika wa kubaki Simba ambao ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Meddie Kagere raia wa Rwanda na viungo, Clatous Chama wa Zambia na Pascal Wawa kutoka Ivory Coast.

“Katika orodha ya wachezaji wa kigeni wanaobaki, Kagere na Chama hawakuwa na pingamizi kuendelea kubaki kuitumikia Simba, Niyonzima kocha hakumtaka si kwa kiwango, bali alidai ni msumbufu lakini uongozi umesema hapana naye atabaki, bado utata upo kwa Wawa, Kotei na Zana,” kilibainisha chanzo chetu.

Kotei alijiunga na Simba wakati wa dirisha dogo Desemba 2016, wakati Wawa ambaye aliwahi kucheza Azam kabla ya kutimkia El Merrikh ya Sudan alijiunga Simba Juni 2018. Zana alitua Simba Novemba 2018 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

“Bado haijaamuliwa kama wachezaji hao wabaki au waachwe, hasa Kotei ambaye aliibua mjadala mzito juu ya hatima yake,” kilisema chanzo chetu kikisistiza kwamba bado nyota hao wako 50-50 kuendelea kuitumia Simba.

Kauli ya Magori

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Simba Sports Club, Crescentius Magori alipoulizwa kuachwa kwa wachezaji saba na usajili mpya wa klabu hakukataa wala kukubali zaidi ya kuhoji mwandishi amezipata wapi habari hizo.

“Hizi taarifa za usajili bado ni za ndani, wewe umezitoa wapi,” alihoji Magori na kufafanua kwamba kuanzia jana jioni wangeweka wazi wachezaji watakaowaongezea mkataba.

“Tutakapomaliza wale ambao tunawaongezea mikataba mipya na ambao tunawaacha au kuwatoa kwa mkopo, tutageukia wachezaji wapya tutakaowasajili, hivyo mashabiki wetu wajiandae kuanzia leo jioni (jana) usajili wetu utakuwa wazi,”alisema Magori.

Kigogo huyo alisema Simba itasajili nyota wapya kulingana na mahitaji ya timu, wako tayari kutumia pesa yoyote kumsajili mchezaji wanayemtaka. “Hatuwezi kujibana katika bajeti, tutasajili mchezaji tunayemtaka, tuko tayari kutumia fedha yoyote kumleta kikosini mchezaji tunayemhitaji, kwani Simba ya sasa ina mipango ya ubingwa wa kimataifa,” alisema.

Meneja wa Gyan, Juma Ndambile alisema mkataba wa mchezaji huyo unamalizika Agosti, lakini Simba hawajatoa kauli kama wataendelea kubaki naye au vinginevyo.