Kondo ajipanga kushinda ugenini

Dar es Salaam. Kocha wa KMC, Habib Kondo amesema wamejipanga vizuri kuendeleza kasi waliyoianza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini amekiri kuwa mechi yao ijayo dhidi ya Mwadui itakuwa ngumu.

KMC inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita, sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya pili, Dodoma FC (nafasi ya tatu) baada ya kushinda mechi zake mbili za nyumbani mfululizo.

Wiki hii yote, Kondo amewafanyisha wachezaji wake mazoezi katika jua kali ili kuhakikisha wanashinda mchezo wao dhidi ya Mwadui utakaofanyika Septemba 21 kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Kondo alisema lengo la kufanya mazoezi katika jua kali ni kuwazoesha wachezaji wake kukabiliana na hali ya hewa ya jua kali iliyopo mkoani Shinyanga na kuhakikisha wanaendeleza kuvuna pointi hata ugenini na kuzidi kuongoza Ligi Kuu Bara.

“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na kesho asubuhi (leo) tutafanya mazoezi na jioni tutaanza safari ya kuelekea Shinyanga kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mwadui.

“Leo (jana) tumecheza mechi ya kirafiki na Dar City ambayo ipo Daraja la Kwanza na lengo la hii mechi ni kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawakucheza katika mechi mbili zilizopita za ligi ili wapate ufiti katika matayarisho kuelekea Shinyanga,” alisema Kondo.