Kocha wa Simba atua AFC

Muktasari:

Bendera aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Simba kabla ya kukaimu ukocha mkuu enzi za utawala wa Hassan Dalali, amekabidhiwa Machalii hao wa Arachuga ili kuwanusuru kutiririka zaidi huko shimoni.

ARUSHA. WAKALI wa zamani Ligi Kuu, AFC Arusha waliopo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) wana hali mbaya na katika kuhakikisha jahazi linaokolewa wameamua kumpa kazi kocha wa zamani wa Simba, Madaraka Bendera.

Bendera aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Simba kabla ya kukaimu ukocha mkuu enzi za utawala wa Hassan Dalali, amekabidhiwa Machalii hao wa Arachuga ili kuwanusuru kutiririka zaidi huko shimoni.

Awali, timu hiyo ilikuwa chini ya David Nyambere, lakini viongozi wamefanya mabadiliko baada ya kuona chama lao limeganda nafasi ya pili kutoka mkiani kwa muda mrefu huku likishindwa kufurukuta.

Katibu wa AFC, Fredrick Lyimo alisema waliamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona hali mbaya huku kocha akiamua kujiondoa kikosini.

“Tumempa Madaraka timu ili kuinoa kwa mechi zilizosalia za duru la pili la FDL,” alisema Lyimo. Alisema ujio wa Bendera ni juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wanaamini watapata mafanikio.

Naye Gambo alisema kuisaidia AFC ni jukumu lake kutokana na timu inawakilisha mkoa wake katika Ligi ya TFF sambamba na Arusha United, akitaka kuona mkoa huo unakuwa na timu ya Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa upande wa Bendera alisema kiwango walichonacho AFC atajipanga na kujua wapi pa kuanzia kuhakikisha anaepuka makosa na kuisaidia kujinusuru kurudi Daraja la Pili (SDL).