Kocha mpya Yanga aanika mechi za ubingwa, aitaja Simba

Monday October 12 2020
kaze 2 pic

KWA mara ya kwanza, Kocha wa Yanga, Mrundi Cedrick Kaze amezungumza na Mwanaspoti na kuthibitisha alihusika kwenye usajili wa mastaa wapya wa kigeni wa klabu hiyo.

Lakini amesisitiza ubingwa wa msimu huu utaamuliwa kwa tofauti ya pointi na mabao huku akisisitiza anajua cha kufanya kukamilisha kiu ya mashabiki wa Yanga.

Kocha huyo amethibitisha atatua alhamisi saa 4 usiku kwa ndege ya KLM

USHINDANI WA NDANI

“Ushindani wa wachezaji ndani ya Yanga ni mkubwa sana, lakini hata Kocha alichelewa sana na timu haikuwa na maandalizi mazuri ndio maana hata wachezaji hawakujuana vizuri. Lakini kwa uwezo wote wanao na uzoefu wa kutosha na wana motisha wa hali ya juu ndio kitu kinanipa matumaini tutafanya vizuri. “Silali usiku, naangalia video nyingi sana kuona jinsi ninavyoweza kuiboresha Yanga kwa kuusoma uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kundi lote, kuona jinsi tunavyoweza kucheza soka nzuri,”anasema.

“Nashukuru viongozi wamefanya usajili mzuri na siyo kusema hakuna sehemu ya kurekebisha lakini timu hii ni nzuri sana.

Advertisement

VIWANJA VIBOVU

“Kuna viwanja vizuri kama kwa Mkapa, kule Bukoba kwa Kagera. Lakini vingine siyo vizuri na hatutakiwi kuwa na visingizio. Wakisema mechi inachezwa Morogoro lazima ujiandae kwa aina ya mazingira unayokwenda kukutana nayo kwa kuangalia staili yako ya kucheza.”

SIMBA NA YANGA

“Mechi imesogezwa mbele kwasababu ambazo ziko nje ya uwezo wangu, nimekubaliana na uamuzi wa mamlaka, kazi yangu ni kutekeleza kazi yangu kuendelea na mambo mengine.

MAANDALIZI KAMILI

“Makocha wakubwa Ulaya na tafiti zilizofanyika ni kwamba timu ikiwa mpya inahitaji miezi mitatu icheze mpira mzuri. Ndio muda ambao wanaweza kuwa na muunganiko mzuri lakini inaweza kuwa chini ya hapo kulingana na uelewa wa wachezaji.”

STAILI YAKE

“Naamini anayeshinda mechi ni yule anayekaa na mpira muda mrefu, naamini huwezi kunifunga kama huna mpira.

“Nataka timu yangu imiliki mpira, icheze mpira, itengeneze nafasi. Kama tunacheza na timu inayojilinda nataka tucheze, tuwalazimishe wacheze. Nataka timu yangu itawale uwanja, nataka wakati tunacheza timu yangu iwe mbali na goli langu tushinde kwenye upande wa mpinzani, tukae kwenye goli lao.

“Hatuwezi kuwa na mafanikio kama hatutakuwa na nidhamu, lazima wachezaji wawe na nidhamu kwenye mazoezi yote ninayowapa. Nje ya uwanja tutaweka kanuni za jinsi ya kuwahi, mtu asikose mazoezi, kuzingatia muda wa chakula siku ya mchezo na badae ya mchezo, jinsi ya kufanya siku mchezaji akiwa hana mechi.

Kwavile naamini hivyo ndivyo vitatusaidia kufanya vizuri na kufikia malengo yetu. Nataka hawa wachezaji kesho na keshokutwa wanikumbuke niliwajenga. Sichezeshi wachezaji 11 bora uwanjani nachezesha timu bora uwanjani.Sichezeshi jina wala staa, nachezesha timu ambayo italeta mafanikio.

FOMESHENI

“Sina fomesheni moja, huwa nabadilika kutokana na hali halisi nataka wachezaji wazoee mambo tofauti kutokana na wachezaji nilionao, mazingira ya uwanja na aina ya mchezo. Nataka kila mchezo amudu kucheza mifumo miwili mpaka mitatu, ili tukikubaliana jambo lifanyike kwa haraka kupata ushindi.

“Hatutaki yale mambo ya kupoteza muda, tumeona kwenye mpira wa Afrika wachezaji wanalala, wanajiumiza, wanapoteza muda sitaki hiyo kwenye timu yangu kwavile mwisho wa siku refa anaongeza muda mwingi halafu unajikuta kwenye matatizo mengi wakati ungeshamaliza mchezo mapema kabisa,”anasema Kaze huku akiwasifu makocha wa Kiafrika.

VLADMIR NA MWAMBUSI

Akiwazungumzia Kocha wa Makipa wa Yanga, Vladmir Niyonkuru na Kocha Msaidizi Juma Mwambusi anasema; “Vladmir nimecheza naye na nimemfundisha pia, ni miongoni mwa makocha wazuri wa makipa Afrika, anajua kazi yake na kupeleka ujumbe kwa wachezaj.

“Mwambusi ni kocha mzuri nimezungumza nae nimemuona, alibeba ubingwa akiwa na Hans Pluijm ni mtu mzoefu na tunatumia uzoefu wake na ubora wake kuirudisha Yanga levo za juu.”

Advertisement