Kocha Yanga aukubali mziki wa Ruvu

KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael amesema miongoni mwa timu bora ambazo amekutana nazo tangu amekuja hapa nchini kufundisha soka ni Ruvu Shooting ambao alicheza nao mechi ya Ligi Kuu Bara juzi Jumamosi katika uwanja wa Uhuru.
Yanga katika mchezo huo walishinda bao 1-0, lililofungwa na David Molinga katika dakika ya 40 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Ditram Nchimbi, huku pia wakipoteza nafasi kadhaa za kufunga mengine japo muda mwingi walikuwa wanapata wakati mgumu kuipenya ngome ya Ruvu.
Kocha Eymael amesema ukiangalia walivyocheza kwa nidhamu kwenye kushambulia baada ya kuona wapinzani wao wakiwa imara hasa eneo la ulinzi, walibadilisha mbinu na hata bao walilofunga lilitokana na kufanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Ruvu.
"Ilikuwa hivyo hivyo hata kwenye safu yetu ya ulinzi kuwazuia washambuliaji wao walionekana kubadilika na kucheza vyema haswa katika kipindi cha pili na kama tusingekuwa makini walikuwa na uwezo wa kutufunga bao la kusawazisha na hata kutoka na ushindi. Ni timu nzuri," alisema.
"Kiujumla Ruvu ni miongoni mwa timu bora na yenye ushindani ambayo nimekutana hapa nchini, ila niwapongeze wachezaji wangu kwa kila mmoja kuweza kujituma katika nafasi yake na kupata pointi tatu ambazo ndio yalikuwa malengo yetu," alisema Eymael.
Yanga inajiandaa kuikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, keshokutwa Jumanne wakiwa na kumbukumbu ya kushindwa kutambiana mjini Iringa walipokutana hivi karibuni.