Kocha Yanga amgomea Morrison, mwenyewe afunguka

Muktasari:

  • Winga huyo wa kimataifa wa Ghana, ambaye hivi karibuni ameingia kwenye mzozo na mabosi wa klabu hiyo hadi kufikishana mbele ya Kamati ya Sheria, Hadhi na Haki za Wachezaji, akionekana mwenye hasira aligoma kukaa kwenye benchi na kuondoka uwanjani hapo wakati mchezo ukiendelea.

MAMBO yameanza kuwa magumu kwa winga wa Yanga, Bernard Morrison, ambaye alisusa kukaa kwenye benchi la timu yake baada ya kufanyiwa mabadiliko kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ambayo, Yanga ilichapwa mabao 4-1 dhidi ya Simba.

Winga huyo wa kimataifa wa Ghana, ambaye hivi karibuni ameingia kwenye mzozo na mabosi wa klabu hiyo hadi kufikishana mbele ya Kamati ya Sheria, Hadhi na Haki za Wachezaji, akionekana mwenye hasira aligoma kukaa kwenye benchi na kuondoka uwanjani hapo wakati mchezo ukiendelea.

Habari ambazo Mwanaspoti ilizipata ni kwamba, tangu siku hiyo Jumapili ya Julai 12, 2020, Morrison hakurejea kambini na hata kwenye mazoezi ya jana Jumatatu hakuwepo.

Lakini, mapema leo Julai 14, 2020 Kocha wa Yanga, Luc Eymael amelieleza Mwanaspoti kwamba, winga huyo amempigia simu kuomba kurejea mazoezini.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Ubelgiji, akagomea ombi hilo na kumtaka Morrison kusubiri kwanza ili apate muda wa kuwasiliana na viongozi kufahamu hatua inayotakiwa kuchukuliwa.

"Kweli, amenipigia simu leo asubuhi akiniomba kurudi mazoezini, lakini kitendo alichokifanya sijakifurahia hivyo, nasubiri kwanza uongozi utoe kauli yao juu yake," alisema Eymael.

Yanga imerejea mazoezi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida United, ambayo tayari imeshashuka daraja. Mchezo huo utapigwa kesho Jumatano saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, uongozi wa Yanga kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wake, Wakili Simon Patrick amesema wanafahamu ni hatua gani watazichukua kwa Morrison kutokana na utovu wa niadhamu aliounyesha.

"Msitulazimishe sana kutoa tamko, uongozi unafahamu ni hatua gani utachukua kwa Morrison…bado tunajadili katika vikao vya ndani na tukikamilisha basi mtapewa taarifa. Kwa sasa hatujatoa tamko lolote," alisema.

Jitihada za Mwanaspoti kumtafuta Morrison kuzungumzia uamuzi wake wa kususa kukaa kwenye benchi la timu yake pamoja na kipigo cha Simba, ziliishia kwa winga huyo kujibu ujumbe mfupi wa maneno tu.

"Nitachati na wewe baadaye, kwa sasa niko bize," alijibu winga huyo ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga hasa baada ya kufunga bao la friikiki kwenye Kariakoo Derby ya Machi 8, 2020 ambapo, Yanga iliichapa Simba kwa bao 1-0.