Kocha Simba amaliza ugomvi na Ajibu

Muktasari:

Ajibu ameifungia Simba bao moja tu katika Ligi Kuu msimu huu ambalo lilikuwa ni katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania walioibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba SC, Sven  Vandenbroeck ameeleza kuwa adhabu ya nyota wake Ibrahimu Ajibu itamalizika Jumatatu ijayo hivyo ataweza kujumuika na wachezaji wenzake kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbelgiji huyo, amelizungumzia sakata la Ajibu, leo asubuhi mara baada ya kumalizika kwa  mazoezi ya kikosi chake ambayo yamefanyika kwenye uwanja wao wa Mo Simba Arena, uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.
Vandenbroeck alisema  kosa la Ajibu ni kuchelewa mazoezini na sio jambo lingine
"Ajibu alichelewa, nikiwa kama kocha nikawajibika kumrudisha nyumbani ikiwa ni sehemu ya kumuadhibu. Nadhani anaweza kurejea kikosini Jumatatu," alisema kocha huyo.
Katika mazoezi ya leo, Vandenbroeck alionekana kuendelea kufanyia kazi utimamu wa miili ya wachezaji wake kwa kuendesha mazoezi mbalimbali ambayo  yalionyesha wazi  kuwajenga wachezaji wake.
Kuna muda walionekana wakikimbia mbio fupi na ndefu huku mchezaji mmoja mmoja akiwa na mpira na muda mwingine bila mpira miguuni.
Kuhusu kutokuwepo kwa Clatous Chama, Sharaf Shiboub na Francis Kahata, Vandenbroeck alitoa ufafanuzi huku akisema Chama na Kahata wanaweza kurejea chini mwanzoni mwa wiki ijayo lakini changamoto ipo kwa Shiboub kutoka Sudan.
"Sudan marufuku yao ina mkazo sana katika kipindi hiki cha corona lakini Kenya na Zambia walau kuna nafuu, tunawategemea Chama na Kahata kuungana nao wiki ijayo," alisema kocha huyo mwenye miaka 40.
Vandenbroeck alizungumzia pia viwango vya utimamu wa wachezaji wake kuwa haviko vibaya licha ya kuwa kila mmoja alikuwa akifanya mazoezi binafsi akiwa nyumbani kwa kipindi cha miezi miwili kutokana na janga la virusi vya corona.
"Kibaya ni kuwa hatujui tutacheza lini mchezo wetu wa kwanza hivyo ni ngumu kupanga ratiba zetu ipasavyo za kujiandaa, lakini kila kitu naamini kitaenda vizuri," alisema.