Kocha Tanzania Prisons kuanza na washambuliaji

Friday November 9 2018

 

By OLIPA ASSA

KOCHA wa Prisons, Abdallah Mohammed 'Bares' anasubiria kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, ili kusajili washambuliaji wazoefu wa kuzifumania nyavu, tofauti na ilivyo sasa ambapo wanamiliki mabao saba katika mechi 13 walizocheza.
Bares alikiri na kuweka wazi kwamba kama kuna safu ambayo imemyumbisha tangu msimu huu kuanza ni safu ya mbele iliyoshindwa kuzalisha mabao mengi ingawa hata ukuta wake umeruhusu  mabao 12.
Katika mechi 13 ambazo Prisons wamecheza wameshinda mchezo mmoja, wametoka sare saba na kufungwa mechi sita ambapo wamejikuta wakiambulia pointi pointi tisa na kuwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi kuu.
"Nafasi ya kwanza ambayo ndio nitakayoelekezea nguvu katika usajili wa dirisha dogo ni ya ushambuliaji kwani ndio ilikuwa na mapungufu mengi zaidi, ingawa lazima niangalia kwa umakini hata eneo la ulinzi.
"Upepo kwetu si mzuri kwani tumefanya vibaya ingawa wachezaji wanaonyesha uhitaji wa kufanya kitu, lakini kadri tunavyocheza hatufiki kwenye malengo yetu,"alisema.
Katibu wa timu hiyo, Abdallah Havimtishi, alisema katika usajili wa dirisha dogo watamsikiliza kile anachokihitaji kocha na tayari wametenga fungu maalumu kwa ajili ya hilo.
"Kama viongozi inatuuma sana kwani nafasi tuliopo sio yetu, yaani mechi 13 tumeshinda moja tu, jana Alhamisi tumeshindwa kusafiri kurejea Mbeya tumeamua kufanya kikao cha dharula cha namna ya kuondokana na hii hali.
"Kesho (Leo Ijumaa) ndio tutaanza safari ya kurudi Mbeya, ila hali hii inatufedhehesha kiasi kwamba tunahitaji kutuliza vichwa namna ya kujinasua hasa tukiongozwa na mahitaji ya kocha wetu Bares,"alisema.

Advertisement