Kocha Pochettino, Raul wawekwa akiba Madrid

MADRID, HISPANIA .MABOSI wa Real Madrid wameripotiwa kuanza kuwawazia Mauricio Pochettino na Raul kama makocha wanaofaa kukabidhiwa mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Bernabeu watakapomfuta kazi Zinedine Zidane.

Ripoti za kutoka Hispania zinafichua kwamba rais wa Real Madrid, Florentino Perez anaamini makocha hao wawili mmoja wao atakuwa chaguo bora kwenye kumbadili Ufaransa Zidane huko Bernabeu.

Kinachosemwa ni kwamba Perez anadhani Raul, ambaye ameshinda mataji 16 katika miaka 16 aliyodumu Santiago Bernabeu ni chaguo sahihi zaidi. Kwa sasa Raul amerejea kwenye kikosi hicho akinoa kikosi cha akiba, Real Madrid Castilla.

Chaguo jingine ni Pochettino, ambaye amekuwa hana timu tangu alipofutwa kazi Tottenham Hotspur, Novemba mwaka jana. Kocha huyo Muargentina amekuwa akihusishwa pia na Manchester United - ambao wamedaiwa wanacheki mwenendo wa kocha wao wa sasa Ole Gunnar Solskjaer.

Kocha, Pochettino alisema mwezi uliopita kwamba ndoto zake ni kuja kuwa kocha wa Real Madrid siku moja. Zidane amekuwa kwenye presha kubwa baada ya mechi sita tu kwenye msimu huu mpya.

Real ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Shakhtar kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huku timu hiyo ikiwakosa wachezaji wake 10 mahiri. Kipigo hicho kimekuja siku nne baada ya kuchapwa kwenye La Liga, walipopigwa 1-0 na timu iliyopanda daraja ya Cadiz. Madrid leo itawakabili Barcelona.